
MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema Mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi walifanya maamuzi ya kupiga kura kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea wa Urais hivyo wanaoongea pembeni wanapaswa kukaa kimya kwa sababu wao sio wanachama. Anaripoti Apaikunda Mosha. Arusha … (endelea).
Gambo ameyasema hayo leo tarehe 19 Februari 2025, Jijini Arusha wakati wa hafla ya Uhamasishaji wa kutoa Elimu ya Nishati Safi kwa Viongozi wa Baraza la Wazee Arusha ambapo ametumia fursa hiyo kueleza Maendeleo ya Jimbo la Arusha Mjini.
“Kama kuna mtu anadhani kwamba hii kazi ni nyepesi, anapoteza muda. Matendo ya Rais Samia yanaishi, yanaonekana na tunalazimika kumwongezea miaka mitano ili kazi hii iwe ya kudumu. Hatuhitaji mtu wa kuja kujifunza au mtu wa kupiga porojo, tunahitaji mtu ambaye anajua anachopaswa kufanya na tayari ameshaanza kufanya,” amesema Gambo.
Amesema kuwa Rais Samia anastahili kuongezewa miaka mitano ya uongozi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kwa ufanisi kwani kazi anayofanya inaonekana na matokeo yake ni dhahiri
Aidha, ametumia fursa hiyo kupitia kampeni ya Rais Samia ya nishati safi kutoa jumla ya majiko ya gesi 182 kwa viongozi wa Baraza la wazee la Arusha ili waweze kulinda mazingira yetu na kutoa Elimu ya nishati safi kwa jamii inayowazunguka.
ZINAZOFANANA
Dk. Nchimbi awatangazia kiama wanaosaka uongozi kwa kuchafuana na matamko
Mkuu wa mkoa Mwanza aitisha kikao kumsaka kada wa Chadema
Lissu: Sina ninachokiogopa, nipo tayari kufungwa, hata kufa