February 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali ya Rais Samia yatekeleza miradi lukuki sekta ya michezo

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Neema Msitha

 

SERIKALI imetumia kiasi cha Sh. 31  bilioni kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa uwanja wa Benjamin Mkapa kwa lengo ya uboreshaji wa sekta ya michezo. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Neema Msitha alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya baraza hilo kwa kipindi cha miaka miaka minne ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hasaan kwa vyombo vya habari katika ukumbi wa habari maelezo jijini Dodoma.

Akizungumzia maendeleo na mafanikio kupitia baraza hilo, Neema ameeleza kuwa ujenzi wa uwanja mpya wa michezo Arusha utagharimu Sh. 338 bilioni hadi kukamilika kwake.

Katika kuendelea kutoa maelezo kwa vyombo vya habari, Neema amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa viwanja vya michezo ambapo ujenzi wa uwanja mpya wa michezo Dodoma unaotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni utagharimu Sh. 310 bilioni.

Ameedelea kutaja ujenzi wa viwanja vingine vya michezo kuwa ni pamoja na viwanja vya mazoezi ikiwemo Gymkhana, Leaders Club, TIRDO, Law School na uwanja wa Farasi hadi kukamilika vitatumia Sh. 21 bilioni.

Mafanikio mengine yaliyoyabainisha kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia ni pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa Kanda ya nne wa kupinga dawa na mbinu haramu michezoni uliofanyika Dar es Salaam mwezi Novemba 2024.

Akielezea mafanikio amesema kuwa katika kuwashawishi wawekezaji katika ujenzi wa viwanja vya michezo, Serikali imeondoa kodi ya nyasi bandia, hali iliyosaidia uwepo wa viwanja katika ngazi za Halmshauri na kusaidia vijana wengi kushiriki katika michezo.

Katika kukuza michezo nchini Serikali ya Tanzania imefanikiwa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo wenye jukumu la kuwezesha timu za Taifa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa michezo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo, kununua vifaa vya michezo na kuendeleza vipaji.

About The Author

error: Content is protected !!