February 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Maendeleo ya michezo yaipandisha bajeti ya Wizara ya Michezo

Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha

 

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha amesema maendeleo katika sekta ya michezo yamechangia ongezeko la bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kutoka  kiasi cha Tsh. 35. 44 bilioni hadi kufikia Tsh. 258 bilioni katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25. Anaripoti Apaikunda Mosha. Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari  leo tarehe 18 Februari 2025, Neema amesema kupitia ongezeko hilo asilimia zaidi ya 200 zimeenda katika miradi ya maendeleo na ukarabati wa miundombinu ili iwe ya kimataifa.

Amesema kuwa baadhi ya miundombinu ya michezo iliyofanyiwa ukarabati ni pamoja na uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo umetumia kiasi cha Tsh. 31 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya uboreshwaji wa  uwanja huo.

Hata hivyo serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa viwanja vikubwa vya kimkakati, uwanja wa Dodoma wenye thamani ya Tsh. 310 bilioni pamoja na kiasi cha Tsh. 286 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa michezo Arusha ambao utajumuisha michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu ambao utakuwa uwezo wa kuingia watazamaji  32 ,000.

Ameeleza mafanikio makubwa ambayo nchi yetu imeyapata ni pamoja na kuwa wenyeji wa mashindano ya kimataifa ya mpira wa miguu ambayo ni Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) na Mataifa ya Afrika (AFCON), ambayo Tanzania itashiriki na kuwa wenyeji ifikapo tarehe Agosti mwaka huu na mwaka 2027.

Aidha amesema kuwa serikali imeondoa kipengele cha tozo kwenye viwanja vyenye nyasi bandia ili kuhamasisha  na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wadau mbalimbali ili waweze kutengeneza viwanja binafsi, na baadhi yao kama Namungo JKT na KMC wameshafanikiwa katika ujenzi wa viwanja hivo.

Aidha ameeleza juu ya zoezi la uanzishwaji wa mfuko wa maendeleo ya michezo kwa ajili ya kuziwezesha timu za taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, kuwezesha utoaji mafunzo kwa wataalamu wa michezo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo pamoja na kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali.

About The Author

error: Content is protected !!