
Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema amejiandaa kufungwa na hata kufa lakini atahakikisha kunakuwa na mabadiliko ya Tume ya Uchaguzi kwa lazima kwa sababu Serikali imekataa kufanya madadiliko kwa hiari. Anaripoti Mwandishi Wetu. Manyoni, Singida … (endelea).
Tundu Lissu akiwa Manyoni mkoani Singida leo tarehe 15 Februari 2025, amesema kinachoenda kufanyika ni uchafuzi sio uchaguzi kutokana na fitna na ufisadi ambao umekuwa ukifanywa mara kwa mara dhidi ya vyama vya upinzani wakati wa Uchaguzi.
Amesema kwamba tunahitaji Tume huru ambayo Chaguzi hazitasimamiwa tena na wafanyakazi wa serikali, kwa sababu wakisimamia wanatishwa na ili wasitishwe tume inatakiwa iajiri wafanyakazi wake yenyewe ili wawe Huru kufanya kazi yao kwa uadilifu na Uhuru.
Ameeeleza kuwa Tume huru ina maana kwamba kuwepo na sheria zitakazo kataza wagombea kuenguliwa, daftari la wapiga kura kuandikwa upya kwasababu daftari la sasa lina taarifa ambazo sio sahii, kusiwepo na vurugu wakati wa kufanya kampeni na pia mawakala wachaguliwe na Chama binafsi na sio msimamizi wa uchaguzi.
“Miaka 33 tangu tume ya Nyalali waseme kuwepo na mabadiliko ya katiba, mfumo mpya wa Uchaguzi na wabadilishe sheria za uchaguzi ili nchi iingie kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa lakini CCM na Serikali yao wamekataa kufanya mabadiliko hayo kwa hiari na sisi tutawashurutisha wafanye mabadiliko,” amesema.
Lissu amesema kuwa lazima tuwe na mfumo wa uchaguzi wa haki kwa sababu haki huinua taifa, hivyo bila mabadiliko hayo hakuna uchaguzi.
ZINAZOFANANA
Mkuu wa mkoa Mwanza aitisha kikao kumsaka kada wa Chadema
DCEA yateketeza ekari 336 za mashamba ya bangi Kondoa
Serikali ya Rais Samia yatekeleza miradi lukuki sekta ya michezo