![](https://mwanahalisionline.com/wp-content/uploads/2025/02/1.jpg)
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis
SERIKALI imewahimiza wananchi katika kila kaya kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda ili kuunga mkono jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo tarehe 14 Februari 2025, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amesema pamoja na kulinda mazingira, pia miti husaidia kutoa kivuli ili kuweza kupata manufaa ya moja kwa moja yatokanayo na miti inayopandwa.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdullah Juma aliyetaka kufahamu Serikali imejipanga vipi kuongeza kasi ya upandaji miti ili kulinda mazingira.
Akiendelea kujibu swali hilo Khamis amesema katika kuongeza kasi ya upandaji miti, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara za kisekta na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wadau wengine imeendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi na Sekta Binafsi kupitia kampeni ya kitaifa ya upandaji miti millioni 1.5 kwa kila halmashauri nchini.
Amefafanua kuwa mwaka 2023/24 jumla ya miti milioni 226.97 ilipandwa, kati ya miti hiyo milioni 211.81 ilistawi sawa na asilimia 76.5. Tathmini ya miti iliyopandwa kupitia kampeni hii kwa mwaka 2024/25 inaendelea.
Amesema Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu mazingira na kuhamasisha wananchi kupanda miti kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo kwa mwaka 2024/25 jumla ya miti milioni 150.16 ilipandwa.
Katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar na miaka 60 ya Muungano, Naibu Waziri Khamis amesema kwa mwaka 2024, miti zaidi ya 53 ilipandwa.
Hivyo, Naibu Waziri Khamis amesema kuwa tathmini ya miti iliyopandwa kupitia utaratibu huu kwa mwaka 2024/25 inaendelea kufanyika na ikikamilika itatolewa kwa umma.
Mtaa wa amana siku 7 zilopita wamekata mkungu wenye umri takriban miaka 50 Kuna transporter kaukata ili waingize Lori kubwa TU lipatalo Tani 40 na hapo ni mtaa wa amana dsm ghorofa nambari 17 na serekali ya mtaa ndio iliobariki mpaka ukaktawa huo mti