February 11, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wassira apiga marufuku Chadema kuwatumia vijana Mara

Stephen Wassira

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wassira apiga marufuku vyama vya upinzani kuwatumia vijana mkoa wa Mara kufanya vurugu mikoa mingine. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).

Amesema CCM inamipango mizuri kuhakikisha vijana hao wanatumia nguvu zao kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kujikwamua dhidi ya umasikini.

Wasira amesema  hayo jana, alipokuwa akizindua ofisi ya CCM Kata ya Nyakonga wilayani Tarime, Mkoa wa Mara.

“Tunawaambia vijana wa Tarime wana mvua wanajua na Tarime panalimika, kila kitu kinaota tuwasaidie vijana wa Tarime watumie fursa zilizopo… tunawaambia CHADEMA muache kuja kuchukua vijana Tarime, sisi sio eneo la mapambano, vijana wetu sio wa kukodisha kwenda katika mapambano, nasema kama mzee wa Tarime waache kuja kuchukua vijana wa Tarime,” alisema Wassira.

Wasira amewataka vijana wasikubali kuchukuliwa na kutumika katika vurugu kwa kuwa wakienda huko hupigwa, kuumizwa na hata kupata ulemavu kisha kurudishwa Tarime wakiwa na hali mbaya.

Kwa mujibu wa Wassira, Tarime ukilinganisha na wilaya nyingine za Mkoa wa Mara ina fursa nyingi zaidi, “hapa tuna madini hapa tuna wachimbaji wadogo na tunataka wachimbaji wadogo walindwe wachimbe kwa amani, tunataka wapewe mafunzo ili wachimbe wapate manufaa kutokana na rasilimali iliyowekwa na mungu katika eneo hili.”

Pia aliwataka vijana wa Tarime walime kwa kuwa wanayo ardhi wananchi wengi wa wilaya hiyo wa na ujuzi wa kufuga hivyo wanaweza kuifanya Tarime yote kuwa ya ng’ombe wa maziwa.

“Kila familia ikawa na ng’ombe wawili wawili ikatufanya tukaweza kujenga kiwanda cha maziwa na watu wa Tarime wakawa wanapata pesa moja kwa moja kila mwezi, hayo ndiyo mambo tunayoyafanya kama Chama,” alisema.

Aidha Wassira amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana kufika wilayani Serengeti kushughulikia suala la mahusiano ya wananchi na Hifadhi ya Serengeti.

Alieleza hayo baada ya kupokea kero ya wananchi kuhusu wanyamapori hususani tembo kuvamia makazi na shughuli zao za kilimo.

Hata hivyoalimtaka Waziri husika afike Serengeti, ashughulikie tatizo hilo na kutoa ripoti kwa chama kuhusu hatua zilizochukuliwa.

“Mahusiano ya watu na Tanapa au Gulmet au Ikorongo, hilo nataka kumuagiza waziri wa Maliasili na Utalii aje ashughulikie mahusiano ya watu hao,’’ alisema.

About The Author

error: Content is protected !!