February 11, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Siku nane kumaliza tatizo la maji Tabata, Ukonga, Kinyerezi

 

HATIMAYE tatizo la maji kwa wakazi wa Kinyerezi, Tabata na Ukonga, linatarajiwa kumalizika ndani ya siku nane kuanzia leo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Aidha wananchi wametakiwa kuwa na matanki ya maji ya angalau lita 5000 ili kuhifadhi maji pale inapotokea changamoto ya shida ya maji.

Hayo yameelezwa juzi na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mkama Bwire wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wa habari iliyotembelea maeneo mbalimbali ya maji hususan ujenzi wa Bwawa la Kidunda lililopo mkoani Morogoro.

Beire alisema neema ya Maji kwa wakazi wa Tabata, Segerea na Ukonga, inakuja baada ya Dawasa kutangaza kuanza kusambaza maji safi kwenye maeneo hayo kuanzia Februari 20, 2025.

Alisisitiza kuwa huduma hiyo inakuja baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji wa Bangulo unaogharimu Sh bilioni 36.8 ya fedha za ndani ambao utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 huku ukijumuisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji la lita milioni tisa na ulazaji wa mtandao wa bomba wenye kilomita 108.

 

Kwa mujibu wa Bwire katika mradi huo, kilichokuwa kikisubiliwa ni kuunganishwa kwa mitambo yao na umeme ili ianze kazi na ndani ya siku mbili, wataanza kuwasha mitambo yao kwa ajili ya majaribio.

Aliwataka wananchi kwa kipindi hiki kuwa na subira hadi ifikapo tarehe hiyo tayari kuanza kuyaachia maji

Katika hatua nyingine, Bwire alisema Dawasa imewaomba wateja wake kuwa na tabia ya kuwa na matenki kwaajili ya kuhifadhi maji ili itakapotokea changamoto yoyote waweze kuwa nayo.

Ametoa rai hiyo ili wakazi wawe na maji muda wote kwaajili ya matumizi yao na wasitetereke pale kunapotokea changamoto.

Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kujenga matenki mengine mengi ya kuhifadhi mamilioni ya lita za maji maeneo mbalimbali.

“Mtunzaji wa kwanza ni yule wa nyumbani wito wangu angalau kaya ikiwa na tenki la lita 5000
kwasababu unakua na uhakika wa kutumia hadi siku tatu endapo huduma ya maji ikiwa haipatikani,” amesema.

Kauli ya TEF

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile ameishukuru Dawasa kwa juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu.

Aidha, ametoa rai kwa mamlaka hiyo kuwapeleka viongozi wa Serikali za mitaa katika maeneo ya kuzalisha maji ili kuwa mabalozi kwa wakazi wao.

Bwawa la kidunda

Ziara hiyo ya TEF na waandishi ilianzia katika mradi wa Bwawa la Kidunda lilikoko Morogoro ambalo kukamilika kwake litaondoa changamoto ya ukosefu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Bwawa hilo linajengwa kwaajili ya kutunza maji yatakayozalishwa na kusambazwa pale yatakapopungua katika mitambo ya uzalishaji ya Ruvu Juu na Chini.

DAWASA imesema utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa bwawa la Kidunda umefikia asilimia 27 na kwamba bwawa hilo linaenda kutoa suluhu ya upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

“Mradi huu ulianzishwa mwaka 1961, hata hivyo haukutekelezwa hadi sasa ambapo serikali ya awamu ya sita inatekeleza kwa fedha za ndani,” Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amewaambia Wahariri na waandishi wa habari waliofika kushuhudia ujenzi wa bwawa hilo.

Zaidi ya Sh. 329.46 bilioni zinatumika katika ujenzi wa bwawa la Kidunda ambalo wataalamu wanasema litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 190 za maji. Bwawa hilo litakuwa na tuta lenye urefu wa mita 870 na litakuwa likizalisha 20 MW za umeme utakaounganishwa na gridi ya Taifa.

Ends

About The Author

error: Content is protected !!