
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Malinyi leo Februari 3, 2025 kimeadhimisha miaka 48 tangu kuasisiwa kwake, kwa kufanya maandamano ya amani kuonesha mshikamano na kuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Mwenza wa nafasi ya Umakamu wa Rais Tanzania Bara Dk. Emmanuel Nchimbi, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mgombea wa nafasi ya Urais Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Malinyi, Peter Mkanigalo, alikemea vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaoanza harakati za kisiasa mapema kwa lengo la kukwamisha juhudi za maendeleo. Alisisitiza kuwa nidhamu ya kisiasa ni muhimu ili kuhakikisha maendeleo ya taifa hayakwamishwi na malumbano ya mapema kabla ya uchaguzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba, aliwahimiza wazazi na wananchi kuhakikisha kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanapata chakula chenye lishe bora. Alieleza kuwa utaratibu maalum wa utoaji wa chakula shuleni unapaswa kuzingatiwa bila kuathiri masomo yao, ili kuwaongezea ari ya kujifunza na kuimarisha maendeleo yao ya kitaaluma.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Malinyi, Abdulrahim Hamad, alisisitiza kuwa chama hicho kimeendelea kuwajibika kwa vitendo katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, kwa kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo.
Alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba, akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ni nguzo muhimu ya kuimarisha demokrasia na maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Antipas Mgungusi, alielezea hatua kubwa zilizopigwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo upatikanaji wa umeme katika vijiji ambavyo awali havikuwa na huduma hiyo. Pia alibainisha mafanikio ya miradi ya maji safi na salama inayotekelezwa ili kuimarisha ustawi wa wananchi.
Aidha, alieleza kuwa serikali inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao, bidhaa na huduma muhimu kwa wananchi wa Malinyi.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, wanachama wa CCM, pamoja na wananchi wa Wilaya ya Malinyi, wakionesha mshikamano na azma ya kuimarisha maendeleo katika jamii.
ZINAZOFANANA
CCM yamfukuza aliyepinga uteuzi wa Rais Samia kugombea
Wassira apiga marufuku Chadema kuwatumia vijana Mara
ACT-Wazalendo chaunda Kamati ya Ilani