WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameagiza kurejeshwa kwa vitambulisho 31,000 vya Taifa (NIDA), vilivyotengenezwa chini ya kiwango na kugawia kwa wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Bashungwa ametoa agizo hilo leo, tarehe 13 Januari 2024 wakati akizungumza na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) waliohudhuria mkutano wa utekelezaji mikakati ya mawasiliano 2024/2025-2025/2026.
Bashungwa amesema vitambulisho hivyo vilichukuliwa na wananchi husika lakini vinafutika jambo linaloondoa thamani na umuhimu la kitambulisho hicho.
“Tumeshatambua changamoto iliyojitokeza na tumeifanyia kazi, nimewaagiza watu wa NIDA wavirejeshe vitambulisho hivyo na wahusika watengenezewe vingine bila malipo yoyote, nawaomba wananchi wenye vitambulisho hivyo wajitokeze” amesema.
Waziri Bashungwa amesema wizara yake inawekeza nguvu zaidi katika kutoa taarifa kwa wakati ili upya usipate taharuki.
“Ni haki ya Watanzania kupata taarifa sahihi kwa wakati, ni jukumu letu kutoa taarifa nawaomba wenzetu wa TEF tushirikiane ili kuboresha utendaji kazi wetu na Taifa” amesema.
Amesema alipoingia wizarani alikuta kuna vitambulisho milioni 1.2 vya NIDA ambavyo havijapelekwa kwa wahusika na aliagiza vipelekwe.
“Hadi jana nimeambiwa 400,000 vimechukuliwa, nimeagiza kasi iongezeke ili kila anayestahili vitambulisho hivyo apate kwa kuwa vina umuhimu mkubwa kwa maisha ya kila siku” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema ni jambo jema kwa wizara kushirikiana wanahabari katika mikakati ya mawasiliano kwa kuwa ndiyo njia itakayokuza ufanisi katika maeneo tofauti.
Balile amemuomba Waziri Bashungwa, amsihi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IJP) Camilius Wambura, kufanya vikao mara kwa mara na wanahabari.
“Huko nyuma IJP alikuwa akikutana na waandishi mara kwa mara na kueleza mipango au kutoa majibu ya masuala mbalimbali, hivi sasa utaratibu huo haupo tena, umeanza vizuri lakini usije ukapotea huko mbele” amesema.
Mwisho.
ZINAZOFANANA
NIDA kutoa vitambulisho laki 4, waboresha mfumo
Maria Sarungi apatikana akiwa hai
Malisa: Uchaguzi wa Chadema ni makosa kimkakati