January 9, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Viongozi CWT lawamani kwa matumizi mabaya, kutowalipa wastaafu

Mwalimu Mundilege Mwambungu Asanga

 

BAADHI ya walimu wastaafu wameulalamikia uongozi wa Chama cha Walimu Taifa CWT kwa kushindwa kuwalipa fedha zao za mkono wa kwaheri tangu mwaka 2020 walipostaafu hadi sasa huku viongozi wakifanya ziara mbalimbali kwa kutumia ovyo fedha za chama. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Wakizungumza na MwanaHALISI Online leo tarehe 8 Januari, 2025 wamesema kuwa uongozi uliopo madarakani kwa sasa umekuwa ukitumia fedha vibaya kwa kufanya ziara ambazo hazina tija na kulipa fedha vikundi vya watu kinyume na katiba kwa lengo la kulinda maslahi yao huku wakishindwa kulipa fedha wanazodaiwa na wastaafu kama mkono wa kwaheri.

Akiongea kwa niaba ya walimu wastaafu juu ya madhira wanayokutana nayo walimu wastaafu Mwalimu Mundilege Mwambungu Asanga mwenye Check Namba 6229047, amesema kuwa tangu kustaafu kwao mwaka 2020 hawakulipwa fedha zao na badala yake wamekuwa wakizungushwa na kibaya zaidi wamekuwa wakikutana na kauli mbaya na kukatisha tamaa kutoka kwa uongozi wa kitaifa.

Mwalimu huyo mstafu ambaye amestaafu akiwa anafundisha shule ya msingi Chamwino Ikulu iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma amesema kuwa hakupata fedha zake na ameendelea na madai lakini mpaka sasa bado hajalipwa fedha hizo.

“Mimi ni mwalimu mstaafu ambaye nilikuwa nafundisha shule ya Msingi Chamwino Ikulu iliyopo katika wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma. Nimestaafu mwaka 2020 na sasa naishi Mkoa wa Mbeya katika wilaya ya Kyela, nilitakiwa kulipwa fedha ya mkono wa kwaheri Sh. 340,000 lakini mpaka sasa sijalipwa fedha zangu.

Mwalimu mstaafu kutoka Kyela, Mundilege Mwambungu Asanga akionesha cheti cha hisa 100

“Nikiwa Kyela nimefuatilia kwa katibu wa CWT Wilaya ikashindikana na ikashauriwa nije kudai madai yangu wilaya ya Chamwino na nilivyofika hapa nimeshauriwa niende CWT makao makuu kwani ndio wanaolipa.

“Nimetoka Kyela tangu tarehe 19 Desemba mwaka jana na nimezunguka makao makuu ya CWT sipati huduma na mbaya zaidi baadhi ya viongozi wamekuwa wakinifokea kwa madai kuwa ni kwanini nimekuja makao makuu ya CWT na kulazimika kunipa Sh 50,000 kama nauli ya kurudi Kyela huku nikiwa sina uhakika watanilipa lini.

“Mimi ni mstaafu nimetoka mbali kote huko naishi kwa shida sina hata mahali pa kulala lakini hawanilipi fedha yangu nimemtafuta katibu Mkuu wa CWT Taifa Joseph Misalaba lakini sijafanikiwa kumpata na chenga zimekuwa nyingi hivyo nimekwama hapa Dodoma,” ameeleza mwalimu Asanga.

Jambo lingine ambalo Asanga amelalamikia ni kitendo cha kuwa na hisa 100 ambazo walielezwa kuwa wanaanzisha benki ya walimu lakini mpaka sasa hakuna jambo lolote linaloendelea na kuongeza kuwa kama uanzishwaji wa Benki umeshindikana ni bora warudishiwe hisa zao.

Katika kutaka kujua ukweli wa mambo alitafutwa katibu wa CWT wa wilaya mojawapo katika mkoa wa Dodoma (jina tunalihifadhi) na kutaka kujua utaratibu ukoje kwa wastaafu kwa kupewa mkono wa kwaheri, amesema kuwa ni kweli walimu wastaafu wengi wanadai fedha zao za mkono wa kwaheri huku akieleza kuwa tatizo kubwa ni uongozi wa CWT ambao wao ndiyo walipaji.

Alipotafutwa Kaimu Katibu Mkuu wa CWT Taifa, Joseph Misalaba ili aeleze changamoto ya walimu wastaafu kutolipwa fedha zao za mkono wa kwaheri amesema kuwa ni kutokana na uhaba wa fedha na sasa zimetengwa Sh. 340 milioni ambazo zitaanza kutolewa kwa wastaafu na kila mwezi watalipwa wastaafu 100 na ndani ya miezi mitatu madeni yote yatakuwa yameisha.

“Nikweli walimu wengi wastaafu wanadai lakini ilikuwa ni tatizo la kibajeti ila kwa sasa zipo milioni 340 ambazo zipo katika utaratibu na zitatolewa kwa vipindi vya miezi 3 ambapo kila mwezi watalipwa walimu 100,” amesema Misalaba.

Baadhi ya walimu wachache katika wengi ambao wanalalamikia mkono wa kwaheri ni, Twiba Ahmed Seif aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Msanga mwenye (check namba 6828037), John Likecha Matembo aliyekuwa akifundisha shule ya msingi Segala (check No.5726697), Sophia Lazaro Cheliga mwenye (Check Na 4409830) na Mariam Hamdan Amour mwenye (Check Na.5234585).

About The Author

error: Content is protected !!