WAFANYABIASHARA sita wa jijjni Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni (Kinondoni), wakikabiliwa na mashitaka 68 yakiwamo ya kupotosha mfumo na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh bilioni 2.1. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakama hapo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daisy Makakala akisaidiana na Wakili wa Serikali, Auni Chilamula imewataja washtakiwa hao kuwa ni ndugu wawili, Stanislaus Mushi (27) na Nemence Mushi (29) wote wakazi wa Malamba mawili, Rose Nanga (33) Mkazi wa Kimara B na Marketing Accountant.
Wengine ni, Hussein Mlezi (37) Mkazi wa Kijichi Mbagala Kuu na Mtaalamu wa Kompyuta, Edwin Mark (22) mfanyabiashara na Mkazi wa Yombo Vituka na Salim Salehe (45) mchoraji na Mkazi wa Vinginguti kwa Komba.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhan Rugemarila.
imedaiwa kuwa mashtaka ya kwanza hadi ya 64 ni ya kupotosha mfumo wa TRA, mashitaka matatu ni ya kusajili Namba ya Mlipakodi (TIN), Namba ya Ongezeko la Thamani (VAT) na mashine ya Kielektroniki ya EFD kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja ni la kuisababishia TRA hasara.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili Makakala amedai kati ya Novemba Mosi na Novemba 30, 2024, maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam washitakiwa walipotosha mfumo wa TRA.
Inadaiwa washtakiwa wote kwa kutumia mashine ya kielektroniki ya EFD yenye namba za kusajili 3TZ843058288 mali ya Hadija Songea walitoa risiti mbalimbali za malipo zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni mbili kwa lengo la kupotosha mfumo na Kamishna Mkuu wa TRA kwa kuonesha mauzo tofauti ya Songea.
Katika shtaka la 66, inadaiwa kati ya Juni Mosi na Juni 30, 2024 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, kinyume na kifungu cha 309 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu namba 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022, washtakiwa Mushi, Nanga na Salehe walisajili kinyume na sheria Namba ya Mlipakodi (TIN) kwa jina la Songea.
Pia inadaiwa kati ya Oktoba Mosi na Oktoba 31, 2024, maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, kinyume na sheria washtakiwa walisajili namba ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa jina la Songea.
Pia inadaiwa kati ya Juni Mosi na Juni 30, 2024, maeneo ya Dar es Salaam, washtakiwa Mushi, Nanga na Salehe walisajili mashine ya Kielektroniki ya EFD yenye namba 03TZ843058288 kwa jina la Songea kwa njia ya udanganyifu.
Katika shtaka la 68, inadaiwa kati ya Novemba Mosi na Novemba 30, 2024, maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, washtakiwa Miushi, Mushi, Nanga, Mlezi, Mark na Salehe waliisababishia TRA hasara ya Sh 2,160,310,567.51 ikiwa ni VAT.
Inadaiwa kwa vitendo hivyo ni kinyume na kifungu cha 284 A ya Kanuni ya Adhabu inayosomwa sambamba na Sheria ya Kudhibiti Uhujumu uchumi.
Hata hivyo, washtakiwa baada ya kusomewa mashitaka hayo, hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Januari 20, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
ZINAZOFANANA
Mvua zakatisha mawasiliano kwa wananchi wa Ulanga
Wazazi, walezi chanzo cha unyanyasaji kwa watoto
Shangwe la Mwaka Mpya 2025: Bei za mafuta zaendelea kushuka