January 8, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mvua zakatisha mawasiliano kwa wananchi wa Ulanga

 

MAISHA ya wananchi katika kijiji cha Mzelezi, kata ya Ruaha, wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, yamebadilika ghafla baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mto Ruaha kuhama mkondo wake na kutenganisha barabara kuu inayounganisha kijiji hicho na maeneo jirani ya Ruaha imekatika kabisa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Kutokana na adha hiyo sasa wananchi wanalazimika kutumia usafiri wa pikipiki kuvuka eneo hilo kwa gharama kubwa ya Sh. 5,000 kwa kila safari.

Hofu ya usalama inatawala miongoni mwa wakazi, hasa wazee, watoto, na akinamama wajawazito ambao wanalazimika kuvuka mto kwa mazingira hatarishi. “Tunajitahidi kuvumilia, lakini maisha yamekuwa magumu sana,” alisema Idda Timdole, mkazi wa kijiji hicho.

Adha ya usafiri imesababisha athari kubwa zaidi, ikiwemo kudorora kwa shughuli za kiuchumi. Wakulima wameanza kuuza mazao yao kwa bei ya hasara ili kufidia gharama za usafiri. “Hali hii inaturudisha nyuma, hatuwezi kufanya biashara kama zamani,” alisema Silivisi Kulima, mmoja wa wakulima katika kijiji hicho.

Changamoto hizi zimewafanya viongozi wa eneo hilo kuingilia kati. Mbunge wa jimbo la Ulanga, Salim Alaudin Hasham, ameahidi kugharamia sehemu ya ukarabati wa barabara hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). “Hatua za haraka zinahitajika ili kuhakikisha wananchi hawateseki zaidi, hasa msimu wa mvua unapokaribia,” alisema Hasham.

Kwa upande mwingine, Mhandisi Petro Daud, Meneja wa TARURA wilayani Ulanga, alibainisha kuwa tatizo hili limesababishwa na shughuli za kilimo karibu na kingo za mto, hali ambayo imeathiri miundombinu ya barabara.

Ameeleza kuwa juhudi za muda mrefu zinahitaji elimu kwa jamii na uwekezaji wa serikali. “Kwa sasa, tumetumia zaidi ya shilingi milioni 60 kwa ukarabati wa awali, na tunajitahidi kukamilisha daraja la mto Ikangao ili kurejesha mawasiliano kati ya kata za Ketaketa na Ilonga,” alisema Mhandisi Daud.

Huku changamoto zikiendelea, wananchi wa Mzelezi wanasubiri kwa hamu kuona tatizo hilo likipata suluhisho la kudumu. Kwa sasa, wanalazimika kuishi kwa tahadhari, huku wakikabiliana na hali ngumu ya maisha.

About The Author

error: Content is protected !!