December 17, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yazindua kampeni Tabasamu Tukupe Mashavu

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua msimu wa pili wa kampeni yake inayofahamika kama “Tabasamu Tukupe Mashavu,” ikilenga kutoa fursa kwa wateja wa benki hiyo kufurahia pamoja na wapendwa wao wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki katika Sikukuu za mwisho wa mwaka kupitia punguzo la bei kwenye manunuzi ya huduma mbalimbali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kupitia kampeni hiyo, benki ya NBC inalenga kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo pesa taslimu, vocha za manunuzi pamoja punguzo la bei kwa asilimia hadi 10 kwenye huduma mbalimbali za kijamii na manunuzi ya vifaa vya kielectorinic huku zawadi kubwa kwa mshindi wa jumla ikiwa ni safari ya kitalii ya siku nne visiwani Zanzibar kwa mshindi na mwenza wake au rafiki.

Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo ilifanyika mapema leo makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa benki hiyo wakiwemo kampuni washirika wa kampeni ambao ni kampuni ya PUMA Energies, ABC Emperio, GSM, Johari Rotana, Bravo Coco, Numero Uno na wafanyakazi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Elvis Ndunguru.

“Jina la kampeni, “Tabasamu Tukupe Mashavu,” linakwenda sambamba kiini cha msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, ambapo “Tabasamu” inaashiria furaha inayotokana na uwezo wa kufanya miamala na malipo popote ulipo huku “Mashavu” ni pale unapopata huduma nzuri na za kuridhisha tena kwa kurudishiwa thamani zaidi,’’ alisema Ndunguru.

Mkurugenzi wa Biashara, Elvis Ndunguru

Kwa mujibu wa Ndunguru, kampeni hiyo ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuhamasisha matumizi ya fedha kupitia mifumo rasmi ya kifedha ikitoa fursa kwao kufurahia miamala iliyorahisishwa wakiwa na marafiki, familia, na wapendwa wao katika kipindi cha sikukuu na mapumziko ya mwisho wa mwaka huku wakinufaika kupitia upendeleo wa bei kupitia punguzo la hadi asilimia 10 kwenye manunuzi sehemu mbalimbali kama vile maduka, supermarkets, migahawa na manunuzi ya mtandaoni.

“Tumeandaa zawadi nyingi na nzuri kwa wateja wetu, ikiwa ni pamoja na safari ya kitalii visiwani Zanzibar iliyolipiwa gharama zote kwa mshindi na mpendwa wake, simu janja zinazotikisa sokoni za Iphone 16 kwa washindi wa kila wiki katika kipindi cha kampeni hii. Lakini pia kuna zawadi nyingine nyingi kama vile gift vouchers, laptops, gas coocker, pesa Taslim na zawadi nyingine tofauti zitakazotolewa kila wiki kwa washindi watakaofanya miamala kwa wingi,’’ alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Meneja Biashara kupitia Kadi, wa Benki hiyo, Esnat Hollela alisema ili kushiriki kwenye kampeni hiyo wateja wa benki hiyo wanatakiwa kutumia kadi zao za NBC VISA kufanya miamala kwenye mashine za ATM, Wakala, maduka, vituo vya mafuta,baa, migahawa, Airbnb, safari, hoteli na malipo mbalimbali ya mtandaoni kama vile Netflix, Amazon, na usajili wa mtandaoni.

“Kadri mteja anavyotumia kadi yake na huduma za NBC, ndivyo anavyoongeza nafasi ya kujishindia zawadi. Na kwa mawakala wa NBC na wale wenye mashine za POS za NBC, wanayo nafasi ya kushinda kwa kuongeza idadi ya miamala wanayofanya kwa wateja wao. Kwa mawakala watakaoongeza miamala ya huduma ya NBC Wakala Pesa, watajipatia nafasi ya ushindi kila wiki,’’ alisema

Kwa upande wao kampuni wadau wa kampeni hiyo wakiwemo kampuni ya PUMA Energies, ABC Emperio, GSM, Johari Rotana, Bravo Coco Beach na Numero Uno walisisitiza dhamira yao kupunguza bei kwenye bidhaa zao ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao kwenye kampeni hiyo lengo likiwa ni kutoa unafuu kwa wateja wa benki ya NBC kupata fursa ya kufurahia sherehe za mwisho wa mwaka sambamba na wapendwa wao

About The Author

error: Content is protected !!