WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais- Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Saada Mkuya Salum amesema idadi kubwa ya wanawake wa visiwani Zanzibar walijitokeza kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikilinganishwa na makundi mengine. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Dk. Mkuya ameeleza hayo mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi tarehe 11 Desemba 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo iliyofanyika Zanzibar
Amesema mpaka kufikia siku ya uzinduzi, kuliratibiwa ushiriki wa wadau wote kutoka Zanzibar katika kutoa maoni yao kuhusu dira hiyo .
“Ushiriki wetu kama Zanzibar tuko vizuri sana, lakini Mheshimiwa Rais (Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar) katika uongozi wake tayari tumeanza kuyaishi yale ambayo tunatamani kuyaishi kuelekea 2050, mfano, katika maoni kulizungumziwa namna tunavyoweza kuwa na mfumo wa fedha usio taslimu (cashless economy), na hili tumeanza kulifanya”, amesema Saada.
Aidha amesema kuwa katika kuanza kutekeleza maoni ya Dira 2050, suala la kubadilisha mitaala limepewa kipaumbele kwa kwenda kwenye mitaala ya ushindani ambayo itahakikisha taifa si tu linakuwa na wananchi na vijana wenye kujiweza kitaaluma bali pia wenye ujuzi unaohitajika kwa wakati huu na ujao.
“Ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba tutakuwa pamoja katika kusimamia utekelezaji huu wa dira yetu, lakini kwanza katika hatua baada ya leo, tutahakikisha kwamba tunasimamia na kuratibu maoni ya Zanzibar kuingia kikamilifu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”, amesisitiza Mkuya.
ZINAZOFANANA
Hatua tano za kukamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo
Dira 2050 kuifanya Tanzania kuwa kinara uzalishaji wa chakula Duniani
Majaliwa aahidi uadilifu, weledi na uaminifu uandaaji Dira 2050