WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Ashatu Kijaji amehimiza mataifa yaliyoendelea kuunga mkono juhudi za nchi zinazoendelea ili ziweze kutekeleza kikamilifu agenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Baku, Azerbaijan … (endelea).
Ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Viongozi wa masuala ya Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.
Dk. Kijaji amesema mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa kuunga mkono juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuondokana na matumizi ya nishati chafu.
Katika Mkutano huo aliambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga pamoja na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – katika masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi Dk. Richard Muyungi.
Wakati huo Waziri Dk. Kijaji amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Burn Manufacturing, Caroline Amollo, ambayo inajihusisha na utengenezaji wa majiko ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.
Katika mazungumzo yao, Waziri Kijaji ameishukuru na kuipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wao kwenye nishati safi ya kupikia nchini Tanzania ambayo ni agenda namba moja ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Pia, amemuhakikishia Bi. Caroline kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuipa ushirikiano kampuni hiyo ili iweze kusaidia katika upatikakanaji wa nishati safi ya kupikia nchini.
Kwa upande wake, Caroline ameishukuru Tanzania na ameahidi kuwekeza zaidi kwenye nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha inapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine, Waziri Dk. Kijaji amekutana na kufanya mazungumzo na Rais ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tomorrow, Rei Goffer.
Kampuni hiyo inajishughulisha na masuala ya Teknolojia ambayo inasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta za usafirishaji, mawasiliano, kilimo na uvuvi.
Katika mazungumzo hayo, Dk. kijaji aliyeambatana na Wataalam kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ameikaribisha kampuni hiyo kuwekeza nchini. Ameihakikishia kuwa Tanzania itatoa ushirikiano ambao itahitaji ili kuhakikisha inanufaika na miradi ya Tomorrow.
Kwa upande wake, Rei amemhakikisha Dk. Kijaji kuwa watawekeza nchini hasa kwenye masuala ya ufuatiliaji wa hali ya hewa. Aidha, ameahidi kuwa kwa kuanza watatoa mafunzo kwa TMA.
ZINAZOFANANA
Wakazi wa Mdundwaro waishukuru TASAF kuwajengea nyumba ya watumishi
Tanzania yakosa Bil 9.3 za nyama
Ukraine wakiri kufanya mauaji ya Jenerali wa Urusi na msaidizi wake mjini Moscow