WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mohamed Mchengerwa amesema uchaguzi wa serikali za mitaa si huruma bali ni sheria na kanuni na atakayekwenda kinyume hatasalimika. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).
Mchengerwa alitoa kauli hiyo leo jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea.
Mchengerwa amesema Taifa halipaswi kuweka huruma mbele kwa kuwa lina sheria na kanuni zinazoongoza eneo husika.
“Tusioneane huruma ili tuvunje kanuni au sheria tulizokubaliana zituongoze, huu uchaguzi ni mchakato wa mwaka mzima, sasa watu wasipofuata sheria na kanuni kwa nini turuhusu huruma?” Alihoji
Mchengerwa amesema malalamiko yanayotolewa hivi sasa juu ya mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea ni kuonyesha mafanikio ya wizara hiyo na mwamko wa Watanzania juu ya uchaguzi huo.
“Uchaguzi huu Ndiyo umezungimzwa zaidi kuliko mwingine wowote uliowahi kutokea, kwetu ni mafanikio na kuonyesha wananchi wameanza kuona thamani ya uchaguzi huo ambao hutoa viongozi kuanzia ngazi za chini.
Mchengerwa amesema kuwa viongozi wa vyama vya upinzani wanaolalamikia kuenguliwa kwa wagombea wao wanatoa propaganda na kufanya upotoshaji kwa kuwa maeneo mengi hawakusimamisha wagombea.
Mchengerwa amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) imesimamisha wagombea katika nafasi zote zinazogombewa ambazo ni 80,430.
Amesema katika nafasi hizo vyombo vya upinzani vimesimamisha wagombea 30,977 (asilimia 38.51).
Amesema kutokana na takwimu hizo asilimia 61 yawagombea wa CCM watapigiwa kura ya Ndiyo na Hapana.
“Hakuna uchaguzi ulioshirikisha vyama vya siasa moja kwa moja kama huu kuanzia hatua za mwanzo, kanuni hadi michakato ya uchaguzi. Si wajibu wetu kulazimisha vyama kuweka wagombea” amesema.
Amesema licha ya kasoro mbalimbali lakini vyama vya upinzani vimeweka wagombea wengi kwenye maeneo ya uchaguzi.
Naye mkurugenzi wa uchaguzi (Tamisemi), Angelista Kihaga, amesema hakuna namna ambayo wagombea watapata fursa ya kuwania nafasi hizo kama wanakiuka sheria na kanuni.
“Tujielekeze katika kukuza demokrasia na kuzingatia taratibu tulizojiwekea kinyume na hapo hatutaeleweka” amesema
ZINAZOFANANA
Prof. Kitila: Lissu ameudanganya Umma, hatukupanga mapinduzi
Lissu ataka Chadema mpya kwenye uongozi wake
Wanawake wametoa maoni kiasi kikubwa – Saada Mkuya