Hezbollah imemteua Amin Qassem, kuwa Katibu Mkuu wa kundi hilo, kurithi nafasi ya Hassan Nasrallah, aliyeuawa na majeshi ya Israel, mwezi mmoja uliopita. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Nasrallah aliuawa mwishoni mwa Septemba, baada ya uvamizi wa Israel ambao ulilenga makao makuu ya Hezbollah yaliyopo Kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Naim Qassem ni nani?
Qassem ameteuliwa kwa kuzingatia kanuni za kundi hilo, akitokea wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Hezbollah, chama cha kisiasa, kijeshi na kijamii ambacho kina msingi maarufu na ushawishi mkubwa miongoni mwa jamii ya Washia nchini Lebanon.
Naim bin Muhammad Naim Qassem, alizaliwa Februari 1953 katika eneo la Basta al-Tahta mjini Beirut.
Ameoa na ana watoto sita, wa kiume wanne na wa kike wawili.
Ni msomi wa ngazi ya juu ya masomo ya kidini, chini ya wanazuoni mashuhuri wa Kishia huko Lebanon. Mbali na elimu ya kidini, Naim pia amesomea shahada ya kemia katika Chuo Kikuu cha Lebanon mwaka 1971.
Katibu huyo mkuu, ni msomi shahada ya uzamili ya kemia katika Chuo Kikuu cha Lebanon mwaka wa 1977.
Amewahi kufanya kazi kama mwalimu kwa madarasa ya sekondari ya umma kwa miaka sita.
Amesoma vitabu vingi vya Kiislamu, ambavyo vilimpatia uzoefu wa kuzungumza hadharani na kuandaa masomo ya kidini katika umri mdogo.
Mwanzoni mwa miaka ya sabini, alichangia kuanzishwa kwa Muungano wa Wanafunzi wa Kiislamu wa Lebanon na kikundi cha vijana, wakati alipokuwa katika madarasa ya chuo kikuu, kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kuwasilisha mawazo ya Kiislamu ndani ya vyuo vikuu na shule.
Alijiunga na harakati za brigedi za upinzani wa Lebanon (Amal), ilipoanzishwa na Imam Musa al-Sadr mwaka 1974 na alihudhuria mikutano ya kwanza ya kuzindua vuguvugu hilo katika mikoa tofauti ya Lebanon.
Alipanda ngazi na kusimamia mafundisho ya utamaduni, akiwa mmoja wa makatibu wa baraza la uongozi wa Amal.
Alichangia kuanzishwa kwa Jumuiya ya Elimu ya Dini ya Kiislam (Shiite), mwaka 1977 inayojishughulisha na ufundishaji wa masuala ya dini ya Kiislamu katika shule za serikali na za binafsi, kwa kupeleka walimu wa kike na kiume katika kila shule kutoa masomo ya dini katika ngazi zote.
Qassim alishiriki katika kamati za Kiislamu zinazounga mkono Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, ambazo zilijumuisha vikundi vyote vya Kiislamu vilivyokuwa vinafanya kazi wakati huo, na ambazo ziliendesha shughuli za vyombo vya habari, maandamano na mihadhara kuhusu mapinduzi hayo.
Kwa zaidi ya miaka 20, Qassem amekuwa akifanya mihadhara sehemu mbalimbali nchini Lebanon, akizingatia masomo ya kila wiki na mwongozo katika maeneo tofauti ya Beirut.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Hezbollah, akifanyakazi bega kwa bega na marehemu Hassan Nasrallah; na katika baadhi ya matukio alimwakilisha kiongozi huyo.
ZINAZOFANANA
Ukraine wakiri kufanya mauaji ya Jenerali wa Urusi na msaidizi wake mjini Moscow
Lungu akwama kuwania urais Zambia
Wananchi Comoro wafurahia huduma madaktari wakitanzania