TUME ya Madini Tanzania imeendelea kurekodi mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo makusanyo ya maduhuli yanayochochewa na mazingira wezeshi ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini,Mhandisi Ramadhani Lwamo ameyasema hayo leo tarehe 24 Oktoba, 2024 jijini Dar es Salaam.
Ni katika kikao kazi kati ya wahariri na wanahabari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Amesema,tume hiyo iliyo chini ya Wizara ya Madini ilianzishwa mwaka 2017 chini ya Sheria ya Madini Sura ya 123.
Amesema, tume ilianzishwa ikiwa na jukumu la kusimamia shughuli zote zinazohusiana na madini nchini kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 22 cha Sheria ya Madini.
Miongoni mwa mafanikio hayo,Mhandisi Lwamo amesema ni kukua kwa makusanyo ya maduhuli kutoka shilingi bilioni 624.6 mwaka 2021/2022 hadi Sh. 753.8 bilioni kwa mwaka 2023/2024.
“Lengo la makusanyo kwa mwaka 2024/2025 ni shilingi trilioni 1 sawa na wastani wa kukusanya shilingi bilioni 83.33 kwa mwezi.”
Mhandisi Lwamo amefafanua kuwa,makusanyo hayo ni sawa na asilimia 103.16 ya lengo la kipindi husika na ni sawa na asilimia 25.79 ya lengo la mwaka 2024/2025.
Mhandisi Lwamo amefafanua kuwa,mwaka 2021/2022 lengo la makusanyo ya maduhuli ilikuwa ni shilingi bilioni 650 ambapo makusanyo halisi yalikuwa shilingi bilioni 624.6 sawa na asilimia 96.
Aidha, mwaka 2022/2023 lengo la makusanyo lilikuwa Sh. 822.02 bilioni na makusanyo halisi yalikuwa shilingi bilioni 677.73 sawa na asilimia 82.
Vilevile, kwa mwaka 2023/2024 amesema lengo lilikuwa ni kukusanya Sh. 852.12 bilioni na makusanyo halisi yalikuwa Sh. 753.81 bilioni sawa na asilimia 85.
Pia, kwa mwaka 2024/2025 lengo ni kukusanya shilingi bilioni 999.99 na hadi kufikia robo ya kwanza wamekusanya Sh. 257.88 bilioni sawa na asilimia 25.79.
Mhandisi Lwamo amefafanua kuwa, kwa mwenendo wa makusanyo wa maduhuli ambao unaonekana hadi sasa huenda wakafikia lengo la zaidi ya asilimia 100 hadi mwishoni mwa mwaka.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kuwa,sekta hiyo imeendelea kuonesha matokeo chanya katika ukuaji wa kisekta.
Amefafanua kwamba, mwaka 2021 ukuaji wa sekta hiyo ulikuwa kwa asilimia 9.4 huku mchango wa sekta ukiwa ni asilimia 7.2.
Mwaka 2022 amefafanua kuwa,ukuaji wa sekta ulikuwa kwa asilimia 10.9 huku mchango wake ukiwa ni asilimia 9.1.
Mhandisi Lwamo ameongeza kuwa, kwa mwaka 2023 ukuaji wa sekta ulikuwa asilimia 11.3 na mchango wake ulikuwa asilimia 9.0.
Wakati huo huo, Mhandisi Lwamo amesema, jumla ya mipango 1,036 ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini iliidhinishwa kati ya 1,050.
Aidha,jumla ya ajira 19,356 zilizalishwa na makampuni ambapo ajira 18,853 ni za Watanzania sawa na asilimia 97.40, wageni 503 sawa na asilimia 2.60.
Kampuni za Watanzania ziliuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 3.46 ikiwa ni asilimia 91.68 na wageni dola za Marekani bilioni 0.31 sawa na asilimia 8.32.”
ZINAZOFANANA
Chuo Kikuu cha Marekani kutunuku shahada ya Udaktari kwa watanzania wanne
Serikali yatia nguvu ubunifu na utafiti kuzikabili changamoto za uchumi na jamii
Wamilikiwa Jengo la Kariakoo wapandishwa kizimbani kwa mauaji bila kukusudia