WAPIGANAJI wa kundi la M-23, wameuteka mji muhimu wa Kalembe wilayani Masisi na kusonga mbele hadi wilaya ya Walikale mkoani Kivu Kaskazini. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa, Kivu, DR Congo … (endelea).
M-23 waliuteka mji huo jana Jumapili, tukio linalowapa nafasi kubwa waasi hao kuviteka vijiji vyenye utajiri mkubwa wa madini wilayani Walikale.
Mji huo wa Kalembe unaochukuliwa kuwa njia muhimu ya kuelekea katika wilaya yenye madini ya Walikale, umekumbwa na ghasia tangu mwaka wa 2021 wakati M23 ilipoanzisha tena mashambulizi Kivu Kaskazini.
Taarifa zinasema kuwa wapiganaji hao walizilenga kwa makombora ngome za vijana wapiganaji wazalendo jana alfajiri, hali ambayo ilizua hofu kwa maelfu wa raia waliokimbilia vijiji jirani, vilivyopo kilomita chache kutoka eneo la mapigano.
Mashirika ya kiraia, yamesema yana na wasiwasi kutokana na kusonga mbele kwa waasi hao wanaolenga kuviteka vijiji wilayani Walikale.
Tobi Kahangu kutoka shirika la raia wilayani Masisi, amesema: “Hili ni tatizo kubwa kuwaona wananchi wakisumbuliwa na vita hata sehemu walikokimbilia na bila ya serikali kulinda maeneo yanayowapokea wakimbizi. Vita nchini Kongo imezua mzozo mbaya wa afya ya akili na msaada ni mdogo mno.”
Leo asubuhi, mamia ya raia wameonekana kwenye barabara toka Kalembe kuelekea mji mkuu wa wilaya ya Walikale, wakibeba mizigo na mifugo, huku wakiwa hawana chakula wala maji.
“Hali ya maisha yaendelea kuwa mbaya sababu ya kukimbia kila siku, hakuna chakula hasa zaidi wakongwe hawana dawa na sehemu ya kulala.”
Vyanzo visivyoegemea upande wowote, vimesema takribani watu 14 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.
Wakati huo huo, wanaharakati wa haki za binaadamu wamesema wana hofu ya hali mbaya ya kiutu katika eneo lenye vurugu.
Kusudi Mapendo kutoka shirika la CADH, amesema: “Sisi kama watetezi wa haki za binadamu, tunahofia maisha ya wananchi katika eneo la Kalembe sababu njia zote zinazoelekea huko zimefungwa na kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi.”
ZINAZOFANANA
Ukraine wakiri kufanya mauaji ya Jenerali wa Urusi na msaidizi wake mjini Moscow
Lungu akwama kuwania urais Zambia
Wananchi Comoro wafurahia huduma madaktari wakitanzania