December 24, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Vodacom yazindua Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kupeleka huduma mtaani  

 

KAMPUNI ya Mawasiliano na Teknolojia Vodacom Tanzania imezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2024 kwa kaulimbiu ya ‘Huduma Bora Kila Wakati’, ambapo kupitia program maalumu ya Huduma Kitaani imeanza kwa kutembelea Soko la Mabibo jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Lengo kuu la Wiki hii ya Huduma kwa Wateja ni kuimarisha mahusiano kati ya kampuni ya Vodacom na wateja wake, huku ikisisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora unaokidhi mahitaji ya mteja.

Akizungumza katika tukio hilo, Harriet Lwakatare, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, alisema, “Wiki hii ni fursa yetu ya kumshukuru kila mteja aliyekuwa nasi muda wote katika safari hii. Kupitia kaulimbiu yetu ‘Huduma Bora Kila Wakati,’ tunaleta huduma zetu moja kwa moja kwa wateja wetu, kuwasikiliza, na kuhakikisha tunawapatia huduma stahiki.”

Mwaka huu, Vodacom Tanzania imeamua kuwasogezea wateja wake huduma kwa kuwafuata pale walipo kwenye shughuli zao za kila siku na kutatua changamoto zao pamoja na kupokea maoni yao kuhusu huduma za Vodacom. Harakati za huduma kitaani zitafanyika pia katika kanda za Vodacom mikoani na itaenda sambamba na utoaji wa msaada katika hospitali kadhaa ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa Vodacom kuchangia damu.

Mteja wa muda mrefu wa Vodacom Tanzania Plc, George Nyamugali (wa nne kutoka kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Harriet Lwakatare wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yaliyofanyika jumatatu katika Soko la Mabibo jijini Dar es Salaam

Lwakatare aliendelea kusema, “Kwetu sisi huduma kwa wateja siyo tu suala la miamala au masuala ya kiufundi ila pia ni kule kujali wateja wetu na kuhakikisha wanapata huduma zinazowasaidia katika maisha yao ya kila siku. Tunataka wateja wetu watumie mtandao wetu na wafanye biashara zao kwa amani, wakijua kuwa Vodacom ipo kwa ajili yao.”

Katika ulimwengu huu wa kidijitali, umiliki wa simu janja sio anasa tena bali ni hitaji la msingi ili mteja aweze kufaidika na huduma mbalimbali za kidijitali. Watanzania walio wengi wameendelea kuingia katika ulimwengu wa kidijitali hivyo kuhitaji msaada wa jinsi ya kutumia na kunufaika.

“Huduma yetu kwa wateja imekuwa ni huduma inayoendana na mabadiliko ya kidijitali, ambapo tumeendelea kubuni njia nyingi za wateja kutufikia, aidha kupitia simu, WhatsApp, mitandao ya kijamii na kadhalika. Vile vile, tunahakikisha huduma zetu ni jumuishi ili kuwafikia watanzania wote hasa wenye mahitaji maalum kama vile wale wenye changamoto za kuona, kusikia au kutembea. Tumehakikisha tumeweka mifumo inayowapa kipuambele na kuwawezesha kupata huduma inayoendana na mahitaji yao”

Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu yataenda sambamba na kuwatambua watoa huduma kinara wa Vodacom katika maduka, mawakala, kituo cha huduma kwa wateja na kadhalika.

About The Author

error: Content is protected !!