MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema zoezi la uandikishaji kwenye daftari la wapiga kura uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijijni na Vitongoji wilayani humo, linaendelea vizuri na idadi kubwa ya wananchi wamejitokeza kujiandikisha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Amesema wakazi zaidi ya 800,000 wenye sifa ya kupiga kura, wanatarajiwa kuandikishwa.
Akizungumza leo baada ya kutembelea vituo mbalimbali vya uandikishaji wilayani humo, Mpogolo amesema Ilala ina vituo 454 katika Mitaa yote 159.
“Katika vituo vyetu vyote hali ni shwari na salama. Tumepita kwenye mitaa yetu yote, mitaa yote iko salama, polisi wameendelea kuimarisha ulinzi.
Niwahakikishie wana Ilala tutaendelea kuwalinda. Wito wangu kwa viongozi wenzangu ni huu, tuendelee kuungana mkono, tuhamasishe wananchi wote wajiandikishe,” amesema.
Aidha, Mpogolo amewaongoza viongozi wa Jumuia ya Taasisi ya Vyuo Vikuu na kati Tanzania (TAHLISO), kufanya usafi katika mitaa ya Kariakoo na kuhamasisha wananchi na vijana wasomi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha katika daftari hilo.
Usafi ulianzia mataa ya Kamata, barabara ya mwendokasi katika mtaa wa Msimbazi hadi kwenye soko jipya la kimataifa Kariakoo.
Akizungumza na wananchi kwenye kijiwe cha jengo la Simba lililopo mtaa wa Msimbazi, Mpogolo amewaelekeza wanachama wa timu hiyo kwenda kujiandikisha.
Pia, ametoa wito kwa wafanyabiashara kujiandikisha na kushiriki uchaguzi, uliopangwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa Sh. 28 bilioni, ambazo zimejenga upya soko la Kariakoo ambalo liliungua; na kwamba sasa lipo katika hatua za mwisho kufunguliwa.
Rais wa TAHLISO, Zainabu Kitima, amemshukuru Mpogolo kwa kushirikiana nao kuhimiza zoezi la uandikishaji na kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji pamoja kuhimiza usafi wa mazingira.
Wadau mbalimbali wameshiriki usafi huo, wakiwamo polisi, bodaboda, wamachinga, wafanyabiashara na watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala.
ZINAZOFANANA
Mil.600 zatengwa kupeleka umeme Kijiji cha Ijinga – Magu
Wakazi wa Mdundwaro waishukuru TASAF kuwajengea nyumba ya watumishi
Tanzania yakosa Bil 9.3 za nyama