Rais Samia Suluhu Hassan, amesema mfumo mzuri wa ukusanyaji na ulipaji wa kodi, utafanikisha lengo la kujenga uchumi jumuishi na unaokua kwa kasi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Ameyasema hayo leo Ijumaa tarehe 04 Oktoba 2024, alipokuwa akizindua Tume ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi, aliyoiunda hivi karibuni.
Amesema mfumo mzuri utaimarisha ustawi wa watu kwa kuboresha huduma za jamii na kupunguza umaskini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja.
Rais Samia amesema Tume hiyo imeundwa kwa lengo la kufanya tathmini ya mfumo mzima wa kodi, kuimarisha zaidi mfumo huo na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ili kurahisisha usimamizi wa ukusanyaji wa kodi nchini.
Amesema tume itazingatia mrejesho na maoni mbalimbali ya wananchi, wadau wa sekta binafsi na wawekezaji wengine, wakati wa kutathmini mfumo huo.
Rais Samia licha ya uchumi wa nchi kukua kwa kasi, idadi ya watu kuongezeka na mahitaji ya huduma za jamii na miundombinu kukua, bado asilimia 60 ya uchumi wa nchi unatokana na sekta isiyo rasmi.
Aidha, amesema Serikali imedhamiria kujenga mfumo wa kodi unaotenda haki, ambao utamuwezesha kila anayestahili kulipa kodi kufanya hivyo na kutoza kodi zote kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza umuhimu wa nchi kuwa na mfumo wa kodi unaochochea ukuaji wa viwanda na kujenga uchumi jumuishi, unaoiwezesha Serikali kuwa na vyanzo vya uhakika na vinavyotabirika vya mapato.
Rais Samia ameipongeza pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa mwezi Septemba 2024.
Tume hiyo inaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue na baadhi ya wajumbe ni aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Musa Assad, Kamishna Mkuu wa zamani TRA, Rished Bade na Gavana mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florence Luoga.
ZINAZOFANANA
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Ushindi wa Profesa Lipumba wapingwa
Sativa amlipia Lissu fomu ya kugombea Uenyekiti Chadema