HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Taasisi ya Global Peace Network (GPN) pamoja na Tanzania Home Economics Organization- TAHEA), inatarajia kuanza kutekeleza mradi wa utengenezaji wa viungo bandia ikiwamo mikono na miguu ili kuwezesha watu wenye uhitaji wa viungo hivyo kuvipata kwa bei nafuu nchini.
Mradi huo ambao ni wa kwanza kuanza kutekelezwa nchini, unatarajiwa kuanza Machi mwaka 2025 kwa kutengeneza miguu bandia 100.
Akiwasilisha taarifa 2024 kuhusu mradi huo leo tarehe 2 Oktoba, mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari, Mkurugenzi Mkuu wa GPN, Dk. Brian Budgell amesema tayari taasisi hiyo imeanza kutoa mafunzo kwa Watanzania ili kuwa na utaalamu wa kutengeneza viungo hivyo.
“Wataalam waliopatiwa mafunzo namna ya kutengeneza viungo hivyo wametoka sehemu mbalimbali huku wakiwa na taaluma zao mathalani uuguzi au udaktari hivyo anajengewa uwezo wa kutengeneza viungo bandia na namna ya kutoa mazoezi tiba,” amesema.
Amesema kutoka Magu wanafunzi saba wamepatiwa mafunzo hayo, Mbeya wanafunzi watatu wamehitimu, Ilemela ni wanne, Kigoma saba na Dar es Salaam watano.
Mbali na utengenezaji wa viungo hivyo, pia wahitimu hao wamepatiwa mafunzo ya utoaji mazoezi tiba hususani kwa wagonjwa wenye matatizo ya kupooza au kiharusi pamoja na magonjwa mengine.
Aidha, Mratibu wa Mradi huo kutoka Hospitali ya Wilaya ya Magu, Sonia Nyamanga amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu wa wananchi wa wilaya hiyo hasa ikizingatiwa huduma za mazoezi tiba ni za gharama na huhitaji mgonjwa muda mwingine mgonjwa kufuatwa.
Naye Mratibu wa miradi wa taasisi hiyo ya GPN nchini, Kahenga Mawe amesema ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa zaidi ya miaka 15 sasa, umechangia taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma za elimu na afya kwa wananchi.
“Tumefanya tathmini katika hopsitali ya Bugando mguu bandia unauzwa Sh 2.7 milioni, CCBRT na KCMC Sh 2.5 milioni, Ajima wanatoa kwa 700,000, lakini ni matumaini yetu halmashauri ya Magu itatoa huduma hii kwa kiwango Rafiki Zaidi,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari ametoa wito kwa watumishi wote wa halmashauri hiyo pamoja na wakuu wa idara kutoa ushirikiano wa kutoka katika kutekeleza mradi huo hasa ikizingatiwa ni chanzo kimojawapo cha mapato ya halmashauri hiyi.
“Kwanza niwahakikishie ushirikiano wa kutosha kutoka kwetu sisi viongozi kwa sababu huu ni mradi ambao unakwenda kuwakomboa wananchi wetu hasa wa vijijini ambao hawana uwezo wa kupata viungo hivi bandia, lakini pili niwaagize watumishi wenzangu kutoa ushirikiano wa kutoka kwa mradi huu wa kipekee,” amesema.
ZINAZOFANANA
Polisi: Waharifu 2024 wapungua mkoani Songwe
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Mil.600 zatengwa kupeleka umeme Kijiji cha Ijinga – Magu