December 25, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Ulinzi mkali kesi ya ‘Boni Yai’

Boniface Jacob akiwa mahakamani

 

Askari Magereza wameweka ulinzi mkali kumlinda Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo (CHADEMA), Boniface Jacob ‘Boni Yai’, anayekabiliwa na mashtaka mawili, katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Mapema saa tatu asubuhi, gari la Magereza liliwasili katika viunga vya mahakama hiyo, huku Boni Yai akiwa analindwa na askari zaidi ya 10.

Akiwa kizimbani, Boni ameonekana akisikiliza na kunukuu mwenendo wa kesi yake, akiwa amezungukwa na askari Magereza wasiopungua 10, huku wengine kadhaa wakiwa na mitutu ya bunduki wakizunguka juu ya rufu ya mahakama.

Boni Yai amefikishwa mahakamani leo tarehe 1 Oktoba 2024, kwa ajili ya uamuzi mdogo wa zuio la dhamana, liliwasilishwa na upande wa Jamhuri kwa kiapo cha ziada.

Tarehe 23 Septemba, ndiyo siku ambayo ilitajiwa kutolewa uamuzi wa zuio la dhamana, Jamhuri ilipigilia msumari kupinga dhamana kwa kuwasilisha kiapo cha ziada cha Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni (RCO), Davis Msangi.

Baada ya ubishani wa kisheria kati ya mawakili wa Jamhuri, wakiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nasoro Katuga; na wanaomtetea BonI Yai, wakiongozwa na Peter Kibatala, mahakama iliahirisha shauri na kupanga kulitolea uamuzi mdogo leo.

Leo tarehe 1 Oktoba 2024, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswagwa, alitoa uamuzi kwa kukitupilia mbali kiapo hicho na kusema kuwa uamuzi wa dhamana ya Boni atautoa Jumatatu ya tarehe 07 Oktoba 2024.

Boni Yai anashtakiwa kwa makosa mawili, likiwemo kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, tarehe 19 Septemba 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswagwa.

About The Author

error: Content is protected !!