RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kitabu cha Hayati Edward Sokoine: Maisha na Uongozi Wake, kinatoa taswira ya safari ya taifa la Tanzania, huku akitaka viongozi wajifunze maisha ya uongozi uliojaa uadilifu, uaminifu na uchapakazi. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Rais Samia akizindua Kitabu hicho chenye kurasa 499, leo tarehe 30 Septemba 2024, jijini Dar es Salaam amesema Sokoine alitekeleza wajibu wake kikamilifu kama msimamizi wa shughuli za kila siku za serikali katika kipindi kigumu.
“Alisimama imara katika kipindi ambacho nchi ilikumbwa na changamoto za uchumi, uhuba wa chakula, miundombinu duni na changamoto katika sekta ya viwanda na afya pamoja na mambo mengi, aliweka mkazo kuendeleza kilimo kufanya mageuzi kwenye uchumi kwa kuruhusu biashara huria ili kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kitabu hicho, kimetoa mafunzo ya uongozi kutoka kwa Sokoine yanayoonekana wakati chokochoko za Nduli Iddi Amini, zilipozidi hadi akavuka mpaka akakalia sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilizofanikisha dikteta huyo kuiachia ardhi ya Tanzania na kukimbia pia nchi yake ya Uganda.
“Sokoine aliongoza vita ya wahujumu uchumi na madhara yake japo aliofariki kabla hajaona matokeo yake, dhamira yake ilikuwa wazi. Funzo kubwa zaidi kiuongozi kutoka kwa Sokoine ni uaminifu, nidhamu na uchapakazi na hii mimi na vijana wale tunatakiwa kujifunza hapa, sifa ambazo ningependa kuzisisitiza kwa viongozi wa sasa na wajao,” amesema.
Ameongeza: “Sokoine alikuwa mwaminifu sana kwa mamlaka yake ya uteuzi na wananchi, ndio maana haishangazi kwamba alikasimiwa majukumu mengi na makubwa ikiwemo Waziri Mkuu katika umri mdogo. Katika hili tunajifunza kwamba ukiwa muadilifu na mchapakazi huna haja ya kukimbizana na vyeo bali vyeo vitakufuata.”
Rais Samia amesema hayati Sokoine ameacha alama takribani kila sekta aliyopita, akiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Kazi, ambako alisimamia kikamilifu ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
“Hivi karibuni nilipokuwa China, tumeamua sisi na wenzetu Zambia na China, kuikarabati reli hiyo na kuifanya kuwa ya kisasa…reli hii ilikuwa na mchango mkubwa katika vita ya ukombozi Kusini mwa Afrika na ni dhamira yetu kuifufua ili itusaidie katika kutekeleza malengo ya Umoja wa Afrika,” amesema.
Kuhusu kuwawezesha wanawake, Rais Samia amesema Sokoine alikuwa chachu ya kuwaruhusu kujiunga na jeshi.
“Alipokuwa Waziri wa Ulinzi alishauri na ikaridhiwa wanawake waanze kuandikishwa jeshi, hii isingetarajiwa kutoka kwa kijana aliyekulia kwenye jamii ya Kimasai ambayo wakati ule nafasi ya mwanamke ilikuwa chini kabisa…hakutaka mila potofu ziharibu kazi yake, alipambana mpaka wanawake wakaanza kuandikishwa jeshi na leo hii tunawaona maofisa jenarali wapo hadi wanawake na vyeo vyao havipatikani kwa sababu wao ni wanawake bali uwezo wao.”
Akizungumzia mchango wake kwenye kilimo, alisema alitaka kiwe cha kisasa kwa kutumia wataalamu wenye stadi stahiki, hivyo alisimamia uanzishwaji wa chuo kikuu cha Kilimo (SUA), ambacho kimepewa jina lake, na kinazalisha wataalamu wengi wanaoendeleza sekta ya kilimo na mifugo.
Kwenye usafirishaji, Rais Samia ameeleza kuwa Sokoine alijibu matatizo ya wananchi akikumbusha kuanzishwa kwa usafiri katika jiji la Dar es Salaama, wakati huo Shirika la Usafirishaji (UDA), lilipozidiwa kwa kutumia mabasi ya watumishi wa umma, aliyoyaelekeza yatumiwe na UDA, badala ya kuyaegesha.
“Kitabu hiki kina mafunzo mengi ya kusisimua kinatupa fursa ya kurudi nyuma na kujitathmini, hali tuliyokuwa nayo miaka 40 iliyopita na hali yetu ya sasa hatujafika kule tunapotaka kuwa, lakini si haba…bidhaa ambazo wakati ule tuliziona ukiwa nazo ni mhujumu uchumi sasa ni bidhaa za kawaida kwenye maeneo na maduka yetu. Tumepiga hatua si haba,” amesema Rais Samia.
ZINAZOFANANA
Ushindi wa Profesa Lipumba wapingwa
Sativa amlipia Lissu fomu ya kugombea Uenyekiti Chadema
John Tendwa afariki dunia