October 1, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kitabu cha maisha ya JK chaanza kuandikwa

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Institute, Kadari Singo

 

MTENDAJI Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Institute, Kadari Singo, amesema wameanza mchakato wa kuandika vitabu viwili, cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashid Kawawa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, alipokuwa akitoa salamu kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu cha hayati Edward Sokoine: Maisha na Uongozi.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mgeni rasmi, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Kikwete, mawaziri, mabalozi, makatibu wakuu na viongozi waandamizi kutoka sekta binafsi na ya umma.

“Unapozindua rasmi kitabu cha hayati Sokoine, taasisi inaendelea kutoa ushirikiano katika uandishi wa kitabu cha Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Aidha, tunaendelea na ukusanyaji wa taarifa mbalimbali kwa ajili ya uandishi wa kitabu cha hayati Rashid Mfaume Kawawa,” amesema Singo.

Aidha, amesema: Ni matumaini yetu kuwa, hata wewe utakapomaliza muda wako, utaruhusu mchakato wa kukusanya taarifa na kuandaa kitabu chako uanze.

Tunaamini kuwa tuna kumbukumbu nyingi zinaendelea kuhifadhiwa kuhusu uongozi wako.”

Taasisi hiyo imeshiriki kuandika kitabu cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kinachoitwa Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yang una cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa: Maisha Yangu, Kusudio Langu.

About The Author