September 28, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Netanyahu aelekeza ‘kichapo’ zaidi kwa Hezbollah

Siku moja baada ya kuambiwa asitishe vita huko Lebanon, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameliambia jeshi lake kuendelea kupigana kwa “nguvu” yake yote kusambaratisha kile alichoita ni ugaidi. Inaripoti Mitandao wa Kimataifa, Tel Aviv, Israel.

Amejibu pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na washirika 12 wa kimataifa, ofisi ya Netanyahu inasema: “Taarifa kuhusu kusitisha mapigano – sio kweli. Hili ni pendekezo la Marekani na Ufaransa, ambalo hata waziri mkuu hakujibu.”

“Waziri mkuu aliagiza IDF kuendeleza mapigano kwa nguvu yake yote na kulingana na mipango iliyowasilishwa kwake. Pia, mapigano huko Gaza yataendelea hadi malengo yote ya vita yatimie.”

Ofisi hiyo imejibu ombi la jumuiya ya nchi 12, iliyotoa siku 21 kusitishwa kwa vita vya Lebanon ikieleza kuwa hali kati ya Israel na Hezbollah, inaleta “hatari isiyokubalika” ya kuongezeka zaidi kwa vita.

Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa Israel imeshambulia maeneo 75 ya Hezbollah kwa usiku mmoja.
Inasema mashambulizi hayo yalilenga maghala ya silaha, vifaa vya kurushia roketi, majengo ya kijeshi na miundombinu.

Mashambulizi hayo yamesababisha miji kutanda moshi wakati jeshi la Israel linadai kufanya kile inachokiita ‘kusambaratisha na kuharibu uwezo wa Hezbollah na miundombinu ya kigaidi.’

Wakati huo huo, Wizara ya afya ya Lebanon, imesema watu tisa wameuawa na wengine 11 kujeruhiwa katika shambulio la Israel la usiku kucha, mjini Younine Kaskazini-Mashariki mwa Lebanon, karibu na Baalbek.

Awali, wizara hiyo ilitangaza vifo vya watu wengine wanne vilivyotokea eneo la Qana na Aita el Shaab huku mamlaka nchini humo zikisema zinaendelea kufukua vifusi.

About The Author