December 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

GGML yaanika mikakati kuwajengea uwezo wanawake sehemu za kazi

 

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imeahidi kuendelea kuwezesha wafanyakazi wake wanawake kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi, kuwajengea uwezo wa kushika nafasi za juu za uongozi na hata kuwawekea mazingira salama yanayopinga aina zote za ukatili wa kijinsia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ahadi hiyo imetolewa Alhamisi, tarehe 12 Septemba 2024 jijini Dar es Salaam na Mwanasheria Mwandamizi wa GGML, David Nzaligo wakati akichangia mada katika uzinduzi wa program ya ajira sawa ambayo inawalenga wanawake walio kwenye sekta binafsi na kukuza usawa wa kijinsia.

Program hiyo mahususi ambayo imelenga kuwezesha wanawake kwenye sekta binafsi, inatekelezwa na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (International Finance Cooperation -IFC) ambayo ni taasisi tanzu ya Benki ya Dunia inayoshughulikia ukuaji wa sekta binafsi kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri (ATE).

Nzaligo alisema licha ya kuwa sekta ya madini imekuwa ikiongozwa zaidi na wanaume, kwa upande wa GGML imeanzisha sera na taratibu ambazo zinawapendelea wanawake na kuwajengea mazingira salama ya kufanya kazi.

Alitoa mfano kwamba, GGML inashiriki katika programu ya Female Future Tanzania (FFT) inayoratibiwa na ATE kwa kuwadhamini wafanyakazi wake wa kike kusoma na kuhitimu kupitia programu hiyo.

Alisema mbali na FFT, pia GGML imekuwa na sera maalumu ya kuwajengea mazingira salama wanawake wanaojifungua ambapo huwapatia muda malumu wa kunyonyesha ikiwa ni pamoja na kuwapatia huduma za usafiri wa kwenda nyumbani kunyonyesha na kurudi.

“Lakini pia ndani ya kampuni kuna mafunzo na warsha mbalimbali ambazo tumewajengea wafanyakazi wetu kuhakikisha kuwa tunafanya kazi kwa ushirikiano bila kujali jinsia, hali hii imetuwezesha kuwashirikisha wanawake hata katika kazi ambazo zilikuwa zinatawaliwa zaidi na wanaume sasa wanawake wanashiriki,” alisema.

Akizundua program hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dk. Dorothy Gwajima alisema anaamini programu hiyo itaongeza kasi ya kuwafikia wanawake wengi zaidi kwa kuwa mchango wa nguvu kazi ya wanawake unazoroteshwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutojumuishwa ipasavyo katika sekta binafsi.

“Taarifa ya Tanzania – Integrated Labor Force survey ya mwaka 2021 inaonesha asilimia 25 tu ya wanawake wapo rasmi kwenye sekta binafsi. Lakini pia, taarifa ya Soko la Hisa la Dar es Salaam inaonesha ni asilimia 19 ya wanawake amba oni viongozi wa bodi za kampuni zilizoandikishwa katika soko hilo. Kwahiyo bado tupo nyuma, tunatakiwa kuchangamka na uchangamshi wetu uanzie huko kwenye ngazi za msingi”.

“Ni shauku ya serikali kuona program hii inaongeza nguvu katika jitihada za serikali za kuwakomboa wanawake na kuleta usawa kwani itatoa fursa kwa kampuni kujifunza kwa pamoja jinsi ya kuondoa changamoto za kijinsia kwenye maeneo ya kazi,” alisema Dk. Gwajima.

Awali akifafanua kuhusu program hiyo, Mkurugenzi wa IFC kanda ya Mashariki na Kusini Maria Porter alisema program hiyo pamoja na mambo mengine inaweka kipaumbele kwenye ujumuishwaji wa wanawake kwenye sekta rasmi ya fedha ambayo mpaka sasa utekelezaji wake umepunguza pengo la kijinsia kutoka asilimia 9 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3 mwaka 2023.

Aidha, alisema tayari kampuni 20 ikiwamo GGML kati ya 65 zimejiandikisha kushiriki katika program hiyo ambayo inalenga kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwakomboa wanawake na kuongeza mchango wao katika ujenzi wa Taifa.

About The Author

error: Content is protected !!