November 22, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Ujenzi tanki la gesi ya Oryx katika soko la feri waiva

 

MBUNGE wa Ilala na Naibu Spika wa Bunge, Musa Azzan Zungu amesema makubaliano ya kisheria yamefikia zaidi ya asilimia 90 na kampuni ya Oryx Gas Tanzania kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tanki kubwa la kisasa la gesi ambalo litagharimu zaidi ya Sh.300 katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza leo tarehe 14 Septemba 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kuutambulisha mradi huo wa ujenzi wa tanki kubwa la kisasa la gesi, Zungu amesema wafanyabiashara wa kukaanga samaki katika soko hilo hupata hasara ya kununua mitungi ya gesi lakini ni asilimia 45 tu ndio inafanya kazi kutokana na mazingira ya gesi kuganda na kuwa barafu.

“Kutokana na hasara hiyo tumeona uje mradi wa tenki la gesi la jumla ambalo kila mtu atakuwa na luku yake na matumizi yake kwa maana hiyo matumizi ya gesi yatakuwa mazuri lakini kwa gharama nafuu.

“Lakini kikubwa tunaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutunza mazingira yetu, moshi wa kuni na moshi wa mkaa unaharibu mazingira yetu katika nchi yetu hivyo tunaungana na Rais pamoja na wadau wetu.

“Tunawashukuru sana kampuni ya Oryx Gas nchini ambayo imekubaliana kwa pamoja kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kusaidia kundi hili la wafanyabiashara wa kukaanga samaki wapate nishati safi na salama lakini kwa gharama ya fedha wanazotoa,” amesema.

Amefafanua mpaka sasa hatua walizochukua kisheria zimekamilika kwa asilimia 90 na hayo yote wanayofanya ni maelekezo ya Rais Samia kuwatazama wananchi wake kwa jicho la huruma kuhakikisha kila mwananchi anafanya shughuli zake kibiashara kwa gharama ya chini.

“Viongozi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala walifanya jitihada za kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa tanki hilo unatekelezwa na walifanya jitihada za kufanikisha kupatikana kwa eneo la mradi huu. Mradi huu umekuja kwa maslahi mapana ya wafanyabiashara, mazingira na taifa kwa ujumla,” amesema Zungu.

Kwa upande Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Ashelly Mbasha amesema mradi huo ni mkubwa ambao unagharimu zaidi ya 300 hadi utakapokamilika na wanategemea kuuanza mapema iwezekanavyo.

“Tunachokiomba Oryx ni ulinzi wa miundombinu mradi utakapoanza kwani tunaweka miundombinu ya gharama kubwa kwa kuwa gesi inataka usalama mkubwa. Kwahiyo tunaomba ulinzi wa hii miundombinu ili iweze kutusaidia wafanyabiashara wote.

“ Oryx tutaendelea kushirikiana na Serikali na kipekee nimshukuru Mbunge kwani huu ni ubunifu mkubwa ambao amekuja nao, kwa kushirikiana na Serikali ya Manispaa ya Ilala ambayo inakwenda kusababisha soko kuwa safi na litakuwa na usalama wa hali ya juuu.

“Kwa hiyo tunaendelea kumpongeza Rais Samia na kampeni yake hii ya kuhakikisha mpaka mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi. Tunaendelea kuwakaribisha wadau wengine wote kutoka kampuni binafsi,mashirika na taasisi tunafanya kazi pamoja kuhakikisha ajenda ya Rais tunaifikisha pamoja,” amesema Mbasha.

Amesisitiza makubaliano ya awali yameshafikiwa na sasa wako hatua za mwisho na hatimaye kuanza utekelezaji wa mradi hivyo wanashukuru kwa hatua hiyo na kubwa wanaomba ushirikiano wa wafanyabiashara wa soko hilo na wadau ili mradi ukamilike kwa muda uliokusudiwa.

Awali Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto amewaomba wafanyabiashara tupokee mabadiliko kwani tunajua mabadiliko yanachangamoto lakini natumaini watayakubali muda sio mrefu.

“Nawashukuru Oryx ambao wanakuja kuleta msaada wa zaidi ya Sh.milioni 300,” amesema Kumbilamoto na kumpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya kwani siku tatu zilizopita walisaini mkataba wa mradi wa tanki kubwa la gesi ya Oryx.

Aidha, amesisitiza wanachosubiri ni kuanza utekelezaji kwani vibali vyote vimeshakamilika vya kuruhusu mradi huo.

Pia amewaomba wafanyabiashara kuwapa ushirikiano Oryx kwani wanachoangalia ni maslahi mapana ya mji wa Dar es Salaam na kuubadilisha lakini wanaenda na kauli ya Rais Samia ya kuhamasisha nishati safi na hivi sasa dunia inamtambua kama Championi wa mazingira kwahiyo sisi tunawajibu kama wasaidizi wake kumsaidia,

Kumbilamoto amesema mchakato wa kubadilisha mji huo kwa matumizi ya gesi hakuna kipaumbele kingine zaidi ya hicho kwa hiyo amesisitiza ushirikiano.

About The Author