September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wastaafu bandari waipeleka Saccos yao Takukuru

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imetumbukia kwenye kashfa, baada ya viongozi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Kukopa – Harbors Sacco’s Limited – kudaiwa kutafuna taribani Sh. 174 milioni, mali za wanachama wake. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam …(endelea).

Wanaosema wanadai mamilioni hayo ya shilingi, ni waliokuwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo, ambao walistaafu kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2012.

Katika kuidhinisha ubadhirifu huo, viongozi hao wa Saccos wanadaiwa kutupa nyaraka za uthibitisho wa michango ya wanachama wao na vitabu vingine vya hesabu kwenye maji, waliyoyafungulia kwenye ofisi za chama hicho ili kupoteza ushahidi.

Akizungumza na MwanaHALISI wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa wastaafu hao, Joseph Mjokonde ametaja madai yao kuwa ni pamoja na michango ya akiba, hisa na faida.

Amesema, licha ya kutimiza vigezo vya kupatiwa stahiki hizo, uongozi umeshindwa kuwalipa stahiki zao.

Amesema, kwa mujibu wa utaratibu, mwanachama wa Harbours Saccos akishastaafu hupewa muda wa siku 90 ndipo hulipwa stahiki zake.

Anasema, yeye alistaafu mwaka 2018 na alikuwa akichangia Sh. 100,000 kila mwezi.

Amesema, michango hiyo hutegemea na viwango vya mishahara kwa wanachama hivyo wengine huchangia Sh. 50,000 na wengine 100,000 kwa mwezi.

“Fedha hizi hukatwa moja kwa moja na mwajiri ambaye ni TPA pindi anapolipa mishahara. Michango  hukatwa moja kwa moja na kuelekezwa kwenye chama,” anaeleza.

Anaongeza: “Sasa cha ajabu kuanzia mwaka 2012 hadi sasa, viongozi wanasema hawana hela za kulipa wanachama waliostaafu, wakati michango imewasilishwa. Hii maana yake ni kwamba fedha hizo wamezitafuna.”

Harbors Sacco’s Limited, kilianzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kuwezesha watumishi wa umma kujikwamua kimaisha.

Mjokonde anasema, “Tulipoanza kufuatilia kwa nyakati tofauti, viongozi walidai nyaraka za kuthibitisha madai yetu zimeharibika, baada ya kuloa maji. Tulipofuatilia tuligundua waliziharibu kwa makusudi ili kupoteza ushahidi.

“Lakini hilo ni jambo dogo sana. Linaweza kutatuliwa kwa kuwa rekodi za michango hiyo zipo pia kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya TPA na mpaka sasa, kila anayelipwa mshahara, mchanganuo wake wa makato, bado unapatikana.”

Mwenyekiti huyo aliungwa mkono na katibu wake, Dominic Kamote, aliyesema kuwa walianza kufuatilia haki zao kwa uongozi wa Saccos hiyo uliokuwa chini ya Athuman Mkangara na meneja wake, Daniel Mlela. Mpaka sasa, hawajaweza kupata haki zao.

Alisema, hata uongozi wa sasa unaongozwa na Gerald Luselo na meneja wake, Mohamed Abdalah Mwinyi, umekwepa kulipa madai yao.

“Tuliwapeleka kwa uongozi wa TPA, wakati huo mkurugenzi mkuu akiwa Deusdedit Kakoko, aliyeagiza tulipwe mara moja. Lakini tukakwama. Tukaenda kwa mrajisi wa vyama vya ushiriki wilaya ya Temeke, uongozi ukaitwa na kuahidi kulipa baada ya mwezi mmoja. Tukasubiri, lakini hatujalipwa,” amesimulia.

Anasema, “Tumeonana na uongozi wa CCM, mkoa wa Dar es Salaam ambao waliwaandikia barua viongozi wa sasa wa bandari. Tukaonana na mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Dar es Salaam, ambaye aliagiza ufanyike ukaguzi wa kuanzia mwaka 2012 hadi 2020. Jambo la ajabu ni kwamba uongozi wa Saccos ndipo ukadai hauna nyaraka na majibu hayo ni baada ya kupiga danadana nyingi.”

Anasema, baada ya uongozi wa Saccos kubanwa, walitoa nyaraka ambazo zinaonesha wastaafu wanaodai ni 44, na malipo yao ni Sh. 89.7 milioni, jambo ambalo si kweli.

Anatolea mfano wa Mjokonde anayedai Sh. 14 milioni, huku uongozi ukisema anadai 12.9 milioni.

Anasema, yeye mwenyewe amestaafu mwaka 2014 na kwa mujibu wa kumbukumbu zake, anadai Sh. 3.7 milioni.

Hata hivyo, katibu huyo anasema, uongozi wa Saccos umedai kuwa anapaswa kulipwa Sh 2.3 milioni. Anasema, hata Nuru Mkono, ambaye ni mjumbe wa kamati ya kufuatilia madai hayo, anadai Sh 6.8milioni, lakini uongozi wa Saccos unasema, anadai Sh. 4.8 milini.

Anasema, “Kinachouma hata hizo walizosema tunadai hawajalipa, wastaafu wanaendelea kuugua, wanakufa, wengine wanakabiliwa na maradhi mbalimbali, lakini wao hawajali.”

Mwenyekiti wa Saccos ya bandari, Gerald Luselo, amethibitia MwanaHALISI Online kuwapo madai hayo. Anakiri baadhi ya madai ya wanachama ni halali.

Lakini anasema, hawezi kuzungumzia suala hilo kwa undani kwa maelezo kuwa linashughulikiwa na vyombo vya dola, ikiwamo Takukuru.

Alisema, “Ni kweli nalitambua suala hilo, lakini kwa sasa siwezi kulizungumzia kwa kuwa lipo kwenye mikono ya vyombo sheria, ikiwamo Takukuru na taasisi nyingine za serikali.”

 

About The Author