December 26, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mbowe amtaka Samia kuunda tume utekaji watu 200

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kutumia mamlaka yake kwa mujibu sheria ya uchunguzi mahsusi kuunda tume ya kimahakama ya majaji kuchunguza tuhuma za utekaji wa watu zaidi ya 200 ambao wengi wao wanadaiwa kutekwa na vyombo vya dola. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia amemtaka Rais Samia afute kifungu cha 4 (3) sheria ya usalama wa taifa iliyopitishwa na Bunge tarehe 14 Julai 2023 kwani kinatoa haki ya maofisa usalama wa taifa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi kukamata watu wanaowadhania wao wanahatarisha usalama wa nchi.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Alhamisi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchunguzi uliofanywa na chama hicho katika matukio ya utekaji, utesaji na hata mauaji aliyodai yanafanywa na vyombo vya dola.

Amesema tume hiyo ya kimahakama pia inatakiwa kuchunguza tuhuma zote hizo pamoja na kuwasikiliza wahanga na mashuhuda sambamba na kuufuatilia mamia ya watanzania waliouawa.
Aidha, ametoa rai kwa watanzania kukataa kukamatwa kama kuku kwa kupambana na watu wanaojaribu kuja kuwakamata bila utaratibu wala kujitambulisha kuwa wao ni polisi.

“Kataeni, msikae kama maboya, watu wanakuja kwa magari yasiyo rasmi wengine marasta man wanakamata watu… tufike mahali tukatae kukamatwa kama kuku,” amesema.

Aidha, ameendelea mbali zaidi ya kutaja orodha ya askari wanaounda kikosi cha utekaji ambacho awali kiliundwa kupambana na uhalifu lakini sasa Mbowe amesema kinatumika kuteka na kutesa watu.

Ametoa mfano wa viongozi wa Chadema wilayani Temeke ambao ni Deus Soka, Jacob Mlay na Frank Mbise kwamba walitekwa na polisi walipotakiwa kwenda kituo cha Chang’ombe kuchukua pikipiki yao iliyopotea.

About The Author

error: Content is protected !!