October 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Washindi NBC ‘Shinda mechi zako kinamna yako’ walamba mil. 40

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imekabidhi zawadi zenye jumla ya Sh 40 milioni kwa washindi wa kampeni yake ya ‘Shinda mechi zako Kinamna yako’ inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi miongoni mwa wateja wake kupitia uwekaji wa akiba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam… (endelea).

Jumla washindi 45 wamepatikana katika kipindi cha miezi mitatu ya kampeni hiyo ya mwaka mmoja kupitia droo za kila mwezi zilizofanyika Makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam zikihusisha maofisa wa benki hiyo pamoja na wawakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini.

Kupitia kampeni hiyo inayolenga makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ambao ni wateja wa benki hiyo wakiwemo wateja binafsi, waajiriwa, wamiliki wa biashara ndogo na wanafunzi ilishuhudiwa washindi wakiibuka na zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha taslimu, simu za mikononi, ‘laptops’, friji, ‘tablets’ za watoto, bima za afya pamoja na majiko ya kisasa ya kupikia.

“Pamoja na zawadi hizo, mwisho wa mwezi huu (Agosti) tunatarajia kutoa zawadi ya gari moja aina BMW X1 ambayo ni kati ya gari mbili tulizopanga kuzitoa kama zawadi kuu katika kampeni itakayodumu kwa kipindi chote cha mwaka huu,” alisema Moses Senkoro, Mtaalamu wa Masoko benki ya NBC, wakati akitoa tathmini ya miezi mitatu ya kampeni hiyo inayohamasisha tabia ya uwekaji wa akiba miongoni mwa watanzania kupitia taasisi zilizo rasmi.

Akizungumzia droo hizo zinazofanyika kila mwezi Senkoro alisema zinahusisha wateja wote waliokidhi vigezo na masharti wanaohudumiwa na benki hiyo kupitia huduma zake mbalimbali zikiwemo akaunti za Chanua, mahususi kwa watoto ambapo washindi walikabidhiwa zawadi za ‘tablets’ za watoto, Akaunti ya Malengo ambapo washindi walikabidhiwa friji, na Akaunti ya Mwalimu pamoja na akaunti ya Johari, mahususi kwa wanawake ambapo washindi walikabidhiwa zawadi za majiko ya gesi na ‘pressure cooker’.

“Pia tumetoa zawadi ya fedha taslimu hadi kiasi cha sh milioni 2 kwa washindi wetu kupitia akaunti ya Biashara, simu za mikononi aina ya Samsung kwa washindi wetu wa akaunti ya Mshahara, laptops kwa washindi wetu wa akaunti ya Wanafunzi, bima za Afya kwa washindi wa Akaunti ya Kua Nasi mahususi kwa wajasiriamali na zawadi ya fedha taslimu hadi laki 5 kwa washindi wa Akaunti ya Vikundi” alitaja.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa Benki hiyo, Arina Kimaryo aliwasihi wateja mbalimbali wa benki hiyo hususani vijana kutumia vema fursa hiyo iliyotolewa na benki ya NBC kupitia kampeni hiyo ili waweze kunufaika kupitia zawadi mbalimbali zinazoambatana na kampeni hiyo.

“Tunaposema shinda mechi zako kupitia kampeni hii tunalenga kuitumia falsafa ya mchezo wa soka ambao Benki ya NBC ndio wadhamini wakuu wa ligi tatu muhimu hapa nchini ikiwemo Ligi ya Kuu ya NBC.

“Tunaingiza falsafa hiyo kwenye maisha tukiamini kwamba wateja wetu wana ndoto, malengo na maazimio mbalimbali waliyopanga kufanikisha hususani kiuchumi na kijamii ikiwemo ujenzi, kukuza biashara zao, kusomesha watoto na mengine mengi…kupitia kampeni hii tunalenga kuwasaidia kufanikisha hilo,” alisema.

About The Author