December 26, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NFRA yajivunia kufikisha mauzo ya nafaka tani mil. 1.7

 

IMEELEZWA kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, uwezo wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulikuwa kuuza wastani wa tani 50,000 za nafaka, lakini baada ya taasisi hiyo kujengewa uwezo imefikisha hadi tani 1,750,000 kupitia mauzo ya nafaka yanayofanyika ndani na nje ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma… (endelea).

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Dk. Andrew Komba wakati akielezea mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema mafanikio hayo ni pamoja na ujenzi wa maghala ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi nafaka zinazonunuliwa kutoka kwa wakulima.

Amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana uungwaji mkono mkubwa kutoka serikalini kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Waziri wake Hussein Bashe.

“Hii imetokana na kasi ya ukuaji wa taasisi hiyo ambayo imepata mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Pia katika kipindi hicho, NFRA kama taasisi ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 50,000 tu za nafaka,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Komba, baadaye uwezo huo uliongezeka hadi kufikia tani 351,000 baada ya utekelezaji wa mradi wa uhifadhi nafaka wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2018 na kusimam iwa na wizara ya kilimo.

“Baada ya uwekezaji huo kufanyika ikiwemo wa miundombino mbalimbali, uwezo wa uhifadhi wa taasisi umeongezeka hadi kufikia tani 400,000 mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu. Matarajio ya NFRA ni kuwa na uwezo wa kuhifadhi kati ya tani 700,000 hadi 1,000,000 kufikia Juni mwakani yaani 2025,” alisisitiza.

Dk. Komba alisema NFRA kwa sasa imebadilisha mtazamo kutoka kuwa taasisi ya kuhifadhi nafaka pekee na kuwa taasisi ya kufanya biashara ya nafaka baada ya kutosheleza hifadhi ya chakula cha kutosha hapa nchini ili kuzidi kujiongezea uwezo.

“Tuna mipango ya kupanua biashara zaidi ya kuuza nafaka katika nchi za jirani kufikia matarajio tuliyonayo,” alisema na kuongeza kuwa NFRA kama taasisi imewajengea uwezo watendaji wake na kuwapa mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuzidi kuwajengea uwezo katika utendaji wao.

“Taasisi pia imeongeza wigo wa masoko kwa kuwatumia wadau tunaofanya nao kazi nje ya nchi ili kuongeza uchumi wa nchi kupitia fedha za kigeni na biashara inayofanyika,” alisema Dk. Komba na kuongeza kuwa NFRA imejipanga kuwa mkombozi wa mkulima.

Dk. Komba alibainisha kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitatu uwezo wa taasisi yake wa kukopesheka kwa ajili ya uwekezaji umeongezeka kutoka bilioni 50 miaka mitatu iliyopita hadi kufikia bilioni 592, ikionyesha kuwa inaaminika na taasisi za kifedha.

About The Author

error: Content is protected !!