November 24, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chadema wamvaa Mchengerwa vijiji, vitongoji kufutwa Ngorongoro

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali ifute amri kuwaondoa wananchi wote wa Tarafa ya Ngorongoro kwenye ardhi yao kwa kufuta kata, vijiji na vitongoji vyote vya tarafa hiyo kwani kuendelea kutumika kwa amri hiyo kutasabaisha maafa makubwa kwa wananchi hao na kuhatarisha amani ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amri hiyo inatajwa kutolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali namba 673 la tarehe 2 Agosti 2024.

Pia Chadema imeitaka Serikali irudi mezani kuzungumza na wananchi hao ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje – Chadema, John Mrema imesema kabla ya amri hiyo Serikali ilisitisha huduma za kijamii kwa wananchi kwa kuondoa huduma za afya, elimu na kusimaisha miradi yote ya maendeleo kwenye tarafa hiyo.

Katika taarifa hiyo pia Chadema wameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi iheshimu Katiba ibara ya 74 na sheria ya Tume ya Uchaguzi ambazo zimeweka bayana kuwa Tume haitapokea maelekezo kutoka kwa mtu au taasisi yoyote, hivyo irejeshe majina ya wapiga kura kwenye daftari la kudumu la wapiga kura walipojiandikisha kwa mujibu wa sheria.

“Katika hali ya kuonyesha kuwa Serikali ilishafanya uamuzi huo ni kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhamisha taarifa za kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kutoka Ngorongoro na kuzipeleka Msomera Tanga bila ridhaa ya wananchi hao.

“Tunaungana na wananchi wa Ngorongoro na tutakuwa nao bega Kwa bega mpaka watakaporejeshwa kwenye ardhi yao ya asili,” amesema Mrema.

Aidha, Mrema amesisitiza kuwa Chadema itaendelea kushirikiana na mashirika na taasisi mbalimbali kuhakikisha kuwa wananchi wa Ngorongoro wanapata haki ya kuishi kwenye ardhi yao ya asili.

About The Author