November 27, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Soko la bidhaa za Halal lazidi kupanuka duniani

 

UKUBWA wa soko la bidhaa za Halal duniani umeendelea kuongezeka kutoka Dola trilioni 1.2 miaka 10 iliyopita hadi kufikia dola trilioni 2.29 mwaka jana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa leo na mtoa mada Salum Awadh wakati akizungumza kwenye kongamano la pili kuhusu mwenendo, fursa na maendeleo ya soko la bidhaa za Halal duniani wakati wa kongamano hilo ambalo limeandaliwa na MICO Halal International Bureau.

Alisema ongezeko hilo ni kubwa na linaonyesha mwamko mkubwa kwa watu kutumia bidhaa za Halal kwenye maeneo mbalimbali duniani kuanzia kwenye bidhaa na utoaji wa huduma.

Alisema soko la Halal liko kwenye maeneo kuanzia ya chakula, fedha, dawa, mavazi, vyombo vya habari na usafiri.

“Fursa la bidhaa za Halal ni kubwa sana hasa ukiangalia waislamu wanawajibika kutumia bidhaa za Halal na hata wasio waislamu wanaweza kutumia bidhaa za Halal,” alisema.

Alisema watanzania wanapaswa kutumia ongezeko la matumizi ya bidhaa za Halal kama fursa ya kutengeneza fedha kwani soko lake limeendelea kuongezeka siku hadi siku.

“Kwenye soko la OIC pekee kuna soko kubwa sana kwasababu watumiaji wa bidhaa za Halal ni wengi sana. Soko liko kubwa hapa nchini, liko Afrika na dunia nzima soko lipo ni wananchi wenyewe kuchangamkia fursa,” alisema

Alisema serikali imekuwa ikihamasisha watu kupeleka nyama kwenye masoko ya mataifa ya uarabuni kama United Arab Emirates (UAE) na Saudi Arabia ambazo zimekuwa zikizingatia matumizi ya bidhaa za Halal.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam, Shamim Khan, alipongeza MICO Halal kwa kuandaa kongamano hilo ambalo litawasaidia wafanyabaiashara kujua namna ya kuzingatia misingi ya Halal kwenye bidhaa zao.

“Nawapongeza sana MICO Halal kwa kuleta hili kongamano kwasababu tulikuwa tunajua maana ya Halal lakini hatuishi kwa kufuata misingi ya Halal kwa hiyo elimu hii itawezesha sisi tuishi kwa kufuata Halal,” alisema

“Lazima tujue unapokwenda supamaketi unanunua kitu kilichofuata Halal kinakuwa kwenye mwonekano gani na kama kimezingatia hasa misingi ya bidhaa za Halal, lazima tujue kitu gani ni halali na kitu gani ni haramu” alisema

About The Author