September 18, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mabosi TAKUKURU, NIDA, Ikulu waguswa panga pangua ya Samia

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali ikiwemo uteuzi wa katibu tawala wa mkoa na naibu makatibu wakuu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka, viongozi walioteuliwa na kuhamishwa vituo vya kazi ni pamoja na CP. Salum Hamduni ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga.

Kabla ya uteuzi huu, CP. Hamduni alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). CP Hamduni anachukua nafasi ya Prof. Siza Tumbo ambaye amerejea Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA);

Amemteua Ismail Rumatila kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya. Kabla ya uteuzi huu, Rumatila alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA);

Mkuu huyo wa nchi amemteua pia Atupele Mwambene kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia masuala ya elimu.

Kabla ya uteuzi huu, Mwambene alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;

Abdul Rajab Mhinte ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo. Kabla ya uteuzi huu, Mhinte alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu; na Methusela Stephen Ntonda ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kabla ya uteuzi huu, Ntonda alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu.

About The Author