December 26, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NMB kuwanoa wajasiriamali 700, kukabidhi Skuli Kizimkazi Festival 2024

 

KAMATI ya Maandalizi ya Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2024), imetambulisha rasmi wadhamini wa mwaka huu, ikiwemo Benki ya NMB ambayo pamoja na mambo mengine itawanoa wajasiriamali zaidi ya 700 na kukabidhi Skuli ya Maandalizi ya Tasani, iliyopo Sheia ya Tasani, Makunduchi, Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Kizimkazi Festival ni tamasha linalotumika kuzindua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na wadau wa maendeleo, zikiwemo taasisi binafsi, ambalo mwaka huu litazinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, Agosti 18.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa wadhamini hao, Meneja wa Biashara wa NMB Zanzibar, Naima Said Shaame, alisema benki yake itashiriki kwa ukubwa tamasha hilo, kuanzia leo tarehe 12 Agosti 2024 hadi siku ya uzinduzi na hatimaye kufungwa kwa tamasha hilo Agosti 25.

“Tunalichukulia tamasha hili kwa ukubwa na umuhimu wake, Kamati ya Maandalizi inatambua kwamba tumekuwa bega kwa bega na tamasha hili tangu linaanzishwa, tuko nalo na tutaendelea nalo, lakini kwa mwaka huu niseme kama ukubwa wa benki yetu ulivyo, basi ushiriki wetu utakuwa mkubwa pia.

“NMB tunathamini, tunajali na kupambania uchumi wa mtu mmoja na taifa kwa ujumla na tuko hapa kudhamini Kizimkazi Festival kwa sababu ni tamasha linalotumika kunyanyua Uchumi na pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisema Naima.

Alibainisha ya kwamba, katika tamasha hilo kwa mwaka 2024, Benki ya NMB itafanya mambo makuu matatu, la kwanza likiwa ni Mafunzo kwa Wajasiriamali zaidi ya 700, ambao watakuwa wakinolewa juu ya elimu ya fedha, uwekezaji na uimarishaji wa shughuli zao za kijasirimali.

“Pili, kutakuwa na siku maalum iitwayo NMB Day, ambayo itakuwa Agosti 20, siku hiyo kutakuwa na matukio matatu, ambayo ni uzinduzi na kukabidhi Skuli ya Maandalizi ya Tasani, ambayo itakabidhiwa kwa Rais Samia, ambaye ndiye aliyeweka jiwe la msingi Agosti 29, mwaka jana,” alieleza.

Skuli ya Maandalisi ya Tasani iliyopo katika eneo la mita za mraba 467, inajumuisha vyumba vitano vya madarasa yatakayochukua wanafunzi 200, sawa na wanafunzi 40 kila moja, Ofisi ya Mwalimu Mkuu, Ofisi ya Walimu, Wafanyakazi, Stoo, Mifumo ya Kisasa ya Majisafi na Majitaka, pamoja na sehemu ya michezo.

“Ukiondoa kukabidhi na kuzindua Skuli hiyo, mchana wa NMB Day kutakuwa na michezo kwenye Uwanja wa Dimani, na kisha usiku wake kutakuwa na Usiku wa Singeli kwa ajili ya kuwafungulia fursa wasanii wa aina hiyo ya muziki waliopo visiwani Zanzibar.

“Jambo la tatu litakalofanywa na NMB katika Kizimkazi Festival 2024, uwepo wa banda la benki yetu katika Viwanja vya Maonesho, ambalo pamoja na mambo mengine, litatoa Huduma za Kifedha, Elimu za Fedha, taarifa mbalimbali za kibenki kwa wananchi watakaohudhuria kwa siku zote za tamasha,” alisisitiza Naima.

Akitambulisha wadhamini wa tamasha hilo, Mwenyekiti wa Tamasha la Kizimkazi, Mahfudh Said Omar, alimtangaza Mhamasishaji Dotto Magari kuwa Balozi wa tamasha la mwaka huu na kuwa kila mdhamini atakuwa na siku za utekelezaji wa majukumu ya kimkataba lengo likiwa ni kutoa fursa pana kwa wawezeshaji.

Ukiondoa NMB, Mahfudh aliwataja wazamini wenza wa Kizimkazi Festival 2024 kuwa ni pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania, Mwanamke Initiatives Foundation, ASAS, CRDB, NBC, TADB, PBZ, TIB, Infocus Studio, Livestream, DSFA, TAHA, BoT, Tallahassee Community College, Tanzania Unforgettable.

About The Author

error: Content is protected !!