November 24, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Viongozi Chadema wamvaa Samia kamatakamata Bavicha

MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika wamemtaka Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kusitisha hatua zinazofanywa na Jeshi hilo kuzuia maadhimisho ya siku ya vijana duniani yanayoandaliwa na Baraza la Vijana Chadema (Bavicha). Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya ….(endelea).

Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka tarehe 12 Agosti, mwaka huu yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Ruanda Nzove jijini Mbeya huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kauli za viongozi hao zimekuja baada ya kuwepo taarifa ya gari za msafara wa vijana wa Chadema toka Mara, Moshi na Arusha kuzuiwa Kilolo Iringa, kwa kuambiwa kuna maelekezo toka juu huki wakizungukwa na gari za polisi wenye silaha.

Kupitia akaunti yake ya mtandao X zamani Twitter, Mnyika ameandika “Rais Samia Suluhu Hassan ukiwa Amiri Jeshi Mkuu na IGP @tanpol sitisheni hatua haramu zinazofanywa na Jeshi la polisi kuzuia shughuli halali inayofanywa na @bavicha_taifa ya maandalizi ya maadhimisho ya #SikuYaVijana #IWD2024 . Zuiazuia na kamata kamata hii ni kinyume na haki na ni dharau kwa 4R mnazojinasibu nazo. Vijana.”

Aidha, Lissu naye ameandika “Rais Samia usilete mambo ya ajabu ajabu ya Magufuli. Siku ya Vijana Duniani inasherehekewa duniani kote. Kwa nini mapolisi wako wanazuia vijana wa CHADEMA barabarani & kuwakamata? Matumizi ya mapolisi yalimshinda Magufuli, & wewe yatakushinda. Fungua barabara vijana waende Mbeya.

“Kwa vijana wote mlioko & mnaoelekea Mbeya: Na Mimi niko njiani kuja Mbeya kuungana nanyi. Kama ni kuzuiliwa au kukamatwa, & mimi wanizuie au kunikamata. Huu sio wakati kukaa kimya, kuogopa au kuuma uma maneno. Ni wakati wa kusimama & kuhesabiwa. Tupaze sauti kwa nguvu zetu zote,” ameandika Lissu.

Hata hivyo, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Juma Haji akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili jijini Mbeya amepiga marufuku kufanyika kwa maadhimisho hayo na kusisitiza watakaokaidi watachukuliwa hatua.

About The Author