Mataifa ya Kenya, Djibouti, Madagascar na Mauritius yamewasilisha rasmi majina ya watu wanaopendekezwa kuwania uwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) huku jina la January Makamba likiwekwa kando. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Umoja wa Afrika umechapisha majina ya watu wanne wanaowania nafasi hiyo akiwemo Mahamoud Ali Youssouf kutoka Djibouti, Raila Odinga wa Kenya, Richard Randriamandrato wa Madagascar na Anil Gayan raia wa Mauritius na kumaliza fununu kuhusu Makamba aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Taarifa za Makamba kuwania nafasi hiyo, zilianza kuvuma baada ya kuibuka vipeperushi katika mitandao ya kijamii vikionesha Wakenya kumpigia chapuo mbunge huyo wa Bumbuli ambaye siku baadaye alienguliwa kwenye baraza la mawaziri.
Nchi wanachama 55 kutoka mataifa wanachama wa AU zinatarajiwa kukutana katika kongamano la Februari mwaka 2025 kumchagua mrithi wa mwenyekiti wa sasa Moussa Faki Mahamat.
Mwaka huu, nchi wanachama wa EAC zimepewa nafasi ya kutoa mrithi wa Faki, raia wa Chad ambaye amehudumu tangu mwaka wa 2017.
“Mimi ndiye mgombea pekee ninayeweza kuzileta pamoja nchi za Afrika zikiwemo zile zinazozungumza Kifaransa, Kiingereza au Kiarabu.” alisema Youssouf raia wa Djibouti.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 58 amekuwa waziri wa mambo ya kigeni katika taifa hilo dogo la pembe ya Afrika tangu mwaka wa 2005.
“Iwapo nitachaguliwa, lengo langu ni kunyamazisha milio ya risasi katika bara la Afrika.” alieleza katika mahojiano na AFP mwezi uliopita.
Mpinzani wake ni kinara wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani nchini Kenya, Raila Odinga, mwenye umri wa miaka 79, ambaye amejaribu kuwania urais kwa mara ya tano bila mafanikio, mwaka wa 2022 akipoteza dhidi ya Rais William Ruto.
Odinga alitumikia miaka yake mingi katika siasa na uhamishoni, akipigania demokrasia wakati wa utawala wa kiimla chini ya hayati Daniel Arap Moi.
“Tunalenga kuleta ushindi huu nyumbani pamoja na kuwatumikia watu kutoka bara Afrika.”
Alisema Odinga kupitia mtandao wake wa X wakati akiwasilisha maombi yake mwezi uliopita.
Gayan (76), alihudumu katika waziri wa mambo ya kigeni wa Mauritius kati ya mwaka wa 1983 na 1986 ambapo tena alihudumu kati ya mwaka wa 2000 hadi 2003 pamoja na kushikilia nafasi zengine katika wizara ya afya na utali.
Randriamandrato alikuwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Madagascar tangu mwezi Machi hadi Oktoba 2022 kabla ya kufutwa kazi baada yake kupiga kura katika Umoja wa Mataifa kupinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Madagascar imetangaza kama nchi ambayo haiegemei upande wowote katika vita vya Ukraine.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika huudumu kwa kipindi cha miaka minne akiwa na uwezo wa kuwania tena mara moja.
ZINAZOFANANA
Ukraine wakiri kufanya mauaji ya Jenerali wa Urusi na msaidizi wake mjini Moscow
Lungu akwama kuwania urais Zambia
Wananchi Comoro wafurahia huduma madaktari wakitanzania