December 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Rais Samia aagiza kiwanda cha tumbaku kuchangia bima ya afya

 

RAIS Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa Kiwanda cha Sigara cha Serengeti (SCC) na Kiwanda cha kuchakata Tumbaku (MTPL) mkoani Morogoro kuchangia mpango wa Taifa wa bima ya afya kwa wote ili kuwatibu wachache watakaokuwa wanakohoa kwa kutumia asilimia tano ya sigara zinazozalishwa na kiwanda hicho na kusambazwa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Rais Samia ametoa wito huo leo Jumanne wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Kiwanda cha Sigara cha Serengeti (SCC) na upanuzi wa Kiwanda cha kuchakata Tumbaku (MTPL) mkoani Morogoro.

Amesema licha ya mmiliki wa kiwanda hicho, Ahmed Huwel kumueleza kuwa asilimia tano pekee ya sigara itayozalishwa na kiwanda hicho ndio itakayosambazwa nchini na iliyosalia kupelekwa nje, amemuomba Serikali imuwekee tozo kidogo.

“Inayovutwa ndani itakuwa na athari kidogo kwa kuwa sasa kuna bima ya afya kwa wote tutaweka katozo kwa dogo, ili wanaokohoakohoa wapate matibabu bila matatizo,” amesema Rais Samia.

Kauli hiyo ya Rais Samie imekuja wakati takwimu kwenye ripoti hiyo ya shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa tarehe 31 Mei 2022 ilionesha kuwa uzalishaji na matumizi ya tumbaku kila mwaka husababisha vifo vya watu milioni nane duniani na kuchangia kukatwa kwa miti milioni 600 huku hekari 200,000 za ardhi zikitumika, pamoja na tani bilioni 22 ya maji.

Hata hivyo, Huwel ambaye ni mmiliki wa kiwanda hicho amemueleza Rais Samia kuwa watatumia teknolojia mpya ya kukausha tumbaku kwa mionzi ya jua badala ya kutumia kuni ili kuendana na mpango wa serikali wa kulinda mazingira.

Katika hilo, mbali na Rais Samia kumpongeza mmiliki huyo, amemtaka kuhakikisha wanaendeleza mkakati wa serikali wa kutumia nishati safi mbali na kupanda miti pekee.

Pamoja na mambo mengine Rais Samia amesema mauzo ya mazao ya tumbaku mwaka jana yalifikia dola za Marekani 400 milioni kwa viwanda vyote vilivyopo nchini huku sehemu kubwa ikitokana na kiwanda mama cha Mkwawa leaf.

“Tunawashukuru wawekezaji kwa kuongeza mapato ya wakulima wetu kutoka dola za Marekani 1.4 hadi 2.4 kwa kilo ya tumbaku si haba wakulima wamepata soko zuri la kuuza mazao ya tumbaku,” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!