September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Jotoardhi kunufaisha kilimo, ufugaji, wavuvi

 

MJEOKEMIA Mwandamizi wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Ariph Ole Kimani amesema uzalishaji wa nishati jadidifu ya Jotoardhi unaondelea kufanyika nchini utaongeza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Anaripoti Selemani Msuya, Dodoma… (endelea).

Kimani amesema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii, alipotembea banda la TGDC lililopo katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni mkoani Dodoma ambapo yanafanyika maonesho hayo kitaifa.

Amesema Tanzania ina vyanzo vya nishati jadidifu ya jotoardhi ambavyo vinaweza kutoa megawati 5,000, hivyo nishati hiyo itaweza kutumika kwa matumizi ya umeme na sekta zingine kama kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Tupo hapa nanenane kuitangaza nishati hii inavyoongeza mnyororo wa thamani kwenye sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, hivyo tunawaomba wananchi kutembelea banda letu, ili waweze kujifunza faida za nishati hii,” amesema.

Mjeokemia huyo amesema baada ya nishati ya jotoardhi kuzalishwa maji yanayobaki yanaweza kuwa na joto la nyuzi 100 hadi 120 ambayo utafiti umeonesha yanafaa kwa shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi na sio lazima kuyarejesha ardhini.

Amesema mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo kuna miradi mingi ya TGDC, ina tabia ya kuwepo joto dogo, hali ambayo inasababisha mazao yasikauke vizuri, hivyo maji yenye joto la nyuzi 100 hadi 120 linapaswa kutumika kutatua changamoto hizo.

“Kutokana na baridi ya mikoa hiyo inaweza kupunguza ubora wa mazao au kuweka sumu kuvu ambayo ina madhara kwa mlaji, hivyo nishati ya jotoardhi inaweza kutumika katika kipengele cha kukausha,” amesema.

Amesema maji ya jotoardhi yenye joto la nyuzi 100 hadi 120 yanatumika kwenye kilimo cha mbogamboga na maua ambayo yamepandwa kwenye shamba kitalu.

“Kwenye shamba kitalu tunapitisha mabomba yenye joto, hali ambayo itasababisha wadudu waharibifu kushindwa kuhimili. Lakini kubwa zaidi mkulima ataachana na matumizi ya viuatilifu vyenye kemikali ambavyo zinasababisha madhara ya magonjwa mbalimbali,” amesema.

Kimani amesema eneo lingine ambalo linaweza kunufaika na joto la maji ya jotoardhi ni uvuvi ambapo mfugaji ataweza kuongeza joto kwenye samaki hivyo kuongeza uwezo wa kuchakata chakula kwa wingi na kukua kwa haraka.

Mjeokemia huyo amesema pia joto hilo linaweza linatumika kukaushia samaki huku wakiwa na ubora mkubwa.

Amesema joto la jotoardhi linatumika kwenye kutotolesha mayai, hivyo wafugaji wa kuku wataachana na matumizi ya kutumia umeme ambao ni gharama kubwa.

“Ni katika ushahidi huo tunadiriki kusema kuwa uwekezaji kwenye nishati jadidifu ya jotoardhi una faida nyingi kwa sababu unaenda kuongeza mnyororo wa thamani katika sekta nyingi zikiwemo hizo tatu ambazo nimezitaja,” amesema.

Kimani amesema TGDC imefanikiwa kutengeneza shamba kitalu na kutotolesha vifaranga, hivyo wana uhakika rasilimali hivyo ya jotoardhi inaenda kuwakomboa Watanzania kiuchumi na kiafya.

Amesema nishati ya jotoardhi hapa nchini inapatikana katika mikoa ya Arusha, Singida, Dodoma, Manyara, Songwe, Mbeya, Morogoro, Pwani na kwingineko.

About The Author