Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Gwajima amemuagiza Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dk. Nandera Mhando kuhakikisha walezi wa kuaminika katika jamii wanaojulikana kama “Fit Persons” wanapata vitambulisho. Anaripoti Matilda Pater, Dar es Salaam … (endelea).
Ametoa maelekezo hayo jana tarehe 2 Agosti 2024, wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mpango wa malezi mbadala kwa lengo la kuzuia watoto kuishi mazingira hatarishi na kukimbilia mitaani na baadaye katika kikao cha pamoja na walezi hao mkoani Dar Es Salaam.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake kwenye Kata za Mabwepande na Mbweni, Wilaya ya Kinondoni, Waziri Dk. Gwajima amebainisha kuwa walezi hao ambao wapo 1803 nchi nzima ni muhimu kwenye jamii kwani wanasaidia kupunguza tatizo la watoto wa mtaani kwa kudhibiti utoro wa watoto hao majumbani kuanzia ngazi ya mtaa.
“Majibu ya kupambana na changamoto za jamii yapo ngazi ya Serikali za Mitaa kwa ushirikiano wa wadau wote kwa kujadili changamoto hizo katika vikao vyote ikiwemo suala la maadili na ukatili kwa watoto ambalo lisipojadiliwa kama zijavyojadiliwa ajenda nyingine, matokeo yake ni watoto kukimbilia kuishi na kufanya kazi mitaani” amesema Waziri Dk. Gwajima.
Amesema vitambulisho vitawasaidia walezi wa kuaminika kutambulika kwa urahisi kwenye jamii na taasisi mbalimbali na kuwa msaada kwa maafisa ustawi wa jamii katika kurahisisha mawasiliano na kutoa msaada wa haraka kwa watoto walengwa.
Amewaelekeza pia maafisa ustawi na maendeleo ya jamii kuwa na takwimu ya wadau mbalimbali ndani ya jamii ili kuunganisha juhudi zao na za walezi hao na kuwawezesha katika kuinua ufanisi wa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuwapa mafunzo ya kuwajenga zaidi katika huduma hiyo.
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dk. Nandera Mhando amesema, walezi hao ambao hadi sasa wamehudumia watoto 586 nchi nzima kwa miezi saba iliyopita, ni mpango wa Serikali kuhakikisha watoto wanaoishi mazingira hatarishi wanapata msaada na hatimaye kuunganishwa na familia zao au familia zinazotaka kuwaasili na kuwalea kama watoto wao.
Baadhi ya Walezi hao akiwemo Martin na Elmelde Kapela wa Kata ya Mabwepande, wamesema wanawasaidia watoto wanaoishi mazingira duni kwenye jamii yao kupata mahitaji ya msingi lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa kukosa vitambulisho pamoja na uwezo wa kiuchumi.
Ziara hiyo imehusisha pia baadhi ya wadau wanaohusika kwenye ajenda hiyo kutoka Mashirika ya SOS Children’s Village, Railway Children Africa na Global Advocates ambao, wamedhamiria kuendeleza ushirikiano na Serikali kwenye ajenda hii.
ZINAZOFANANA
Polisi: Waharifu 2024 wapungua mkoani Songwe
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Mil.600 zatengwa kupeleka umeme Kijiji cha Ijinga – Magu