November 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwalimu aliyemchapa mwanafunzi kwa madai ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ahukumiwa gerezani

 

MWALIMU wa shule ya sekondari ya Kings iliyopo Goba jijini Dar es Salaam Yusuph Mirambi (43), amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani na kulipa faini ya Sh. Milioni mbili baada ya kupatikana na hatia ya ya kumuadhibu mwanafunzi wake wa kidato cha pili isivyohalali.

Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Veneranda Kaseko wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Julai Mosi, 2024.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Veneranda amesema upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake watano na vielelezo ikiwemo fomu ya polisi namba tatu’pf3′ wameweza kuthibitisha bila ya kuacha shaka kuwa mwalimu Mirambi alitenda kosa hilo.

“Nimepitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashata na ushahidi wa utetezi kutoka kwa mshtakiwa, na hivyo mshtakiwa anatiwa hatiani kwa kosa alilotenda” amesema Hakimu.

Hakimu Veneranda amesema hukumu hiyo imezingatia hoja ya msingi moja kama tukio la viboko limetokea na mshtakiwa ndiye mhusika.

Hakimu veneranda alinukuu ushahidi uliotolewa na baba mzazi wa mwanafunzi huyo, septemba 28 mwaka 2022 kuwa “niliitwa na mkuu wa shule shuleni hapo akitaka kwenda kujadili kuhusiana na nidhamu ya kijana wangu”

Amesema alipofika shule aliambiwa kijana wake anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja hivyo shule inampa adhabu ya kumfukuza.

Alidai alirudi nyumbani na kijana wake lakinikatika siku alizokaa nae mtoto alikuwa analalamika hawezi kukaa ndipo Oktoba 2 mwaka 2022 alifika ofisi za ustawi wa jamii kuomba msaada wa kumsaidia mtoto kwa kuwa anadai anamaumivu na hawezi kukaa pia anasumbuliwa na msongo wa mawazo kwa kitendo cha kuambiwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Pia Katika ushahidi wa daktari kutoka hospitali ya Mloganzila katika uchunguzi wake alibaini makovu yaliyopo katika makalio ya mtoto yanayoenda kupona alipomgusa kijana alipiga kelele za maumivu ndipo alipomchunguza zaidi na kugundua vidonda hivyo vilikuwa centimeta 5.10 kwa ndani na kumpatia dawa za kutuliza maumivu.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mtoto mwenyewe alipoieleza mahakama kuwa hakumbuki idadi ya viboko alivyopigwa na mwalimu huyo kwakuwa vilikuwa vingi vya kupitiliza akimshutumu akiri kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja kutokana na kuzidiwa na maumivu alikiri kwa kuandika barua ambayo iliwasilishwa mahakamani hapo kama kielelezo cha mshtakiwa.

Aliendelea kudai kuwa mwalimu huyo alikuwa akimpiga mara kwa mara mwanafunzi na kushindwa kukaa darasani hivyo alitumia kupiga magoti alipozidiwa aliomba msaada wa kuitiwa mzazi ili wampelekee dawa za kutuliza maumivu kitendo ambacho mwalimu hakukifanya.

Upande wa jamhuri pia umethibitisha shtaka la madai ya mtoto huyo kujihusisha na vitendo hivyo baada ya kuleta kielelezo cha fomu ya polisi namba tatu ‘pf3’ iliyochunguzwa katika hospitali ya palestina ambapo daktari alidai katika uchunguzi wake alibaini mtoto huyo hajawahi kuingiliwa.

Hakimu alisema kitendo cha mtoto kuchapwa kupitiliza ni kosa na kinyume cha sheria ya mtoto inayoelekeza watoto wasipewe adhabu kali kupitiliza na kuwatesa kipindukia kwa kuwaathiri kimwili na kiakili.

Hata hivyo kabla ya hukumu kusomwa Hakimu aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ndipo wakili wa serikali Deborah Mushi alidai hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa na kuiomba mahakama kumpatia adhabu kali.

“Naiomba mahakama impatie mshtakiwa adhabu kali ya juu kabisa kwa mujibu wa sheria kwa sababu kitendo alichokifanya mshtakiwa kwa mtoto huyo ni kitendo cha udhalilishaji na kumsababishia athari kubwa kwa sasa na hata baadaye .

Mshtakiwa alitoa adhabu kali ya viboko na kumhusisha na mapenzi ya jinsia moja mtoto jambapo ambalo athari zake huenda ikajitokeza siku za mbele mfano anaweza kuja kuwa kiongozi mkubwa hata Rais wa baadae ama mwanasiasa itakuja kumtesa kwa mwanafunzi wenzake na jamii pia pale ambapo wanajua anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja mtoto huyo hatapata muda wa kujisafisha na tuhuma hizo ambazo ametengenezewa.

Kwa upande wa mshtakiwa aliwakilishwa na wakili msomi Malieth Molle ambapo aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu mteja wake ambayo imekusudia kuutoa kwasababu mshtakiwa mkosaji wa mara ya kwanza na anasumbuliwa na ugonjwa wa pumu pia ni baba na familia yake inamtegemea.

About The Author