October 31, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kinana ajiuzulu Makamu Mwenyekiti CCM, Rais Samia aridhia

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la kujiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye amemwandikia barua ya kuomba kupumzika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 29 Julai mwaka huu na Katibu wa NEC -Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, Rais Samia ameridhia ombi hilo kwa moyo mzito.

Amesema katika majibu yake Mwenyekiti wa CCM amesema “Ni kweli nilipokuomba utusaidie kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti nilikuahidi utakaa muda mfupi kama ulivyoomba, na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia lakini kwa kuwa umeomba sana na ahadi ni deni nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujiuzulu kwako”.

Pia Mwenyekiti wa CCM amesisitiza kuwa Chama kitaendelea kutumia uzoefu na maarifa ya Kinana kila vitakapohitajika.

“Chama Cha Mapinduzi kinamshukuru Kinana kwa mchango wake mkubwa kwa Chama chetu,” amesema Makala.

Kinana aliteuliwa kushika wadhifa huo kuanzia tarehe 31 Machi 2022 baada ya Philip Mangula naye kujiuzulu nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM bara.

Hata hivyo, Kinana ambaye ni nguli wa siasa nchini tarehe 28 Mei 2018 alijiuzulu nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho tawala CCM, kilichokuwa kinaongozwa na Rais John Magufuli.

About The Author