Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro ameshinda uchaguzi uliofanyika jana Jumapili hatua inayomuwezesha kuongeza muda wa utawala wake kwa muhula wa tatu wa miaka sita. Inaripoti Mitandao wa Kimataifa … (endelea).
Rais wa Tume ya Uchaguzi ya CNE nchini humo, Elvis Amoroso amesema Maduro ameshinda kwa asilimia 51.2 ya kura huku asilimia 44.2 ikienda kwa mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez.
Matokeo hayo yametangazwa katika wakati ambao wapinzani wa Maduro walikuwa wanapanga kuyapinga.
Jana jioni wanasiasa wengi wa upinzani walikuwa wameanza kushangilia kupitia mitandao ya kijamii wakisema mwelekeo uliokuwa unaonesha mgombea wao Gonzalez angepata ushindi wa kishindo.
Matumaini yao yalitokana na uchunguzi wa maoni ya wapigakura kuonesha Gonzalez alikuwa akiongoza na alikuwa na nafasi nzuri ya kuibuka mshindi.
Tume ya uchaguzi ambayo inadhibitiwa na watu watiifu kwa Maduro bado haijachapisha matokeo yote kutoka vituo 30,000 vya kupigia kura.
Upinzani ulisema kwamba unatilia mashaka uhuru wa uchaguzi huo hasa baada ya wafanyakazi wake kadhaa kukamatwa.
Wawakilishi wa upinzani wanasema karatasi za majumuisho ya kura waliyokusanya kutoka kwa mawakala wao wa uchaguzi katika asilimia 30 ya vituo vya kupigia kura zinaonesha Gonzalez alikuwa amemshinda Maduro.
Katika uchaguzi huo wa jana, Maduro alipata upinzani mkali zaidi tangu alipoingia madarakani.
Mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez ambaye ni mwanadiplomasia wa zamani alikuwa na uungwaji mkono mkubwa ikiwemo kutoka kwa nyota wa upinzani Maria Corina Machado ambaye alizuiwa kugombea nafasi yoyote ya kisiasa mwaka jana.
ZINAZOFANANA
Mtaalamu wa kemia kiongozi mpya Hezbollah
Israel yapiga marufuku UN kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina
Israel yaoshambulia Iran kwa njia ya anga