MWANAMUZIKI maarufu katika Muziki wa Injili nchini Rehema Simfukwe amevunja ukimya kwa mara ya kwanza kwa kuamua kutoa sababu za kutunga wimbo wa Chanzo ambao umekuwa ukipendwa na kuvuta hisia za watu wengi kutokana na mashairi yaliyoandikwa katika wimbo huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Rehema Simfukwe tangu alipotoa wimbo huo miaka minne iliyopita hakuwahi kutoa sababu za kutunga na kuimba wimbo huo lakini ameona sasa ni wakati muafuaka kuwaambia Watanzania kuhusu wimbo Chanzo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana usiku wa Januari 12,2024 wakati wa hafla ya kuelezea sababu za kuimba wimbo wa Chanzo sambamba na kusherehekea kumbukizi ya kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza Dorcas ambaye ametimiza miaka sita tangu kuzaliwa kwake.
Amemetumia nafasi hiyo kueleza kuwa Dorcas ndio sababu iliyomfanya yeye kuimba wimbo wa Chanzo kwani ni mtoto ambaye alimzaa na amekuwa na changamoto ya kupooza kwa ubongo au mtindio wa ubongo.
“Mungu amenijaalia watoto watatu lakini duniani huku watu wengi wanajua nina watoto wawili. Mtoto wangu wa kwanza anaitwa Dorcas ambaye alizaliwa na changamoto ya kupooza ubongo au mtindio wa ubongo kwa hiyo alikuwa na changamoto sana katika maisha yake
“Changamoto hiyo kwa Dorcas ilisababisha tangu alipozaliwa tukawa na maisha ya hosipitali siku hadi siku. Nimekuwa nikiimba nyimbo za injili, nafanya mahojiano na vyombo vya habari kuhusu wimbo wa Chanzo lakini sijawahi kueleza upande wa pili kuhusu wimbo huu,” amesema mwanamuziki Rehema Simfukwe.
Amesema amekuwa kimya muda wote kwasababu alikuwa anasubiri apate kibali kutoka kwa Mungu kuzungumzia wimbo huo na hiyo ndio sababu ya kutunga na kuimba wimbo huo ambao unazungumzia maisha halisi ya Mtoto Dorcas.
“Ukiusikiliza wimbo huu utaona ndani yake kuna ujumbe uliobeba maumivu ya Dorcas na ndio sababu ya kuimba wimbo huo, nafahamu tangu ulipotoka watu wameuopokea, na wamekuwa wakiuimba na kuufurahia na nimekuwa nikiulizwa sababu za kuimba wimbo huu.
“ Nilimuahidi Mungu kuwa sitasema hili mpaka pale atakaponiruhusu na nimekaa na hii siri kwa miaka kadhaa na ninaamini Mungu amenipa mtoto Dorcas ili niwe mfano kwa wengine, ili nisaidie wengine wenye watoto wenye changamoto kama za Dorcas.
Hata hivyo amesema wakati wakisherehekea kumbukizi ya kuzaliwa kwa mtoto Dorcas pia ameamua kutangaza kufungua kituo cha kuelea watoto ambao wanachangamoto ya mtindio wa ubongo. Kituo hicho kitafahamika kwa jina la Dorcas Home Care Initiative kilichopo Madale jijini Dar es Salaam.
“Wakati leo tunafurahia miaka sita ya Dorcas naomba nitangaze uwepo wa Dorcas Homecare Initiative, lengo la kituo hiki ni kupokea watoto wenye changamoto ya mtindio wa ubongo, na hakutakuwa na gharama yoyote kwani nimeamua kutoa huduma ya kulea watoto hao na nimeanza na watoto nane.
Kwa wale ambao wataguswa basi wanaweza kutuchangia kupitia akaunti ya NBC 074172000439TZS na 074173000101 wakati namba ya benki ya CRDB ni 015C0005PQW00 TZS na namba ya M-pesa ni 0768571613(Dorcas Home Care, amesema mwanamuziki Rehema Simfukwe.
ZINAZOFANANA
Pesa nyingi zipo leo hii
Suka jamvi lako la ushindi hapa
Kuwa milionea na Meridianbet siku ya leo