October 18, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mambo matano makubwa kuhusu Raila

 

RAILA Amollo Odinga, aliyefariki dunia Jumatano asubuhi nchini India, alikuwa mtu mashuhuri nchini mwake. Ameweka rekodi ya kukuza demokrasia katika maisha ya kisasa yake kwa zaidi ya miongo minne.

Kiongozi huyo mkongwe wa upinzani alifariki akiwa na umri wa miaka 80, alikuwa nchini India, akipatiwa matibabu kutokana na ugonjwa ambao haujawekwa wazi.

Kifo chake sio tu kinaashiria mwisho wa enzi ya mwanamageuzi wa Kiafrika, lakini pia kinaacha pengo kubwa katika upinzani wa Kenya wakati nchi hiyo inaelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Ingawa Odinga alitoka katika familia maarufu ya Kenya, taji la kisiasa lilimponyoka katika kipindi chote cha maisha yake ya miongo kadhaa – kama vile lilivyomkwepa babake, ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais baada ya Kenya kupata uhuru wake kutoka Uingereza. 

Mnamo 2022, Odinga aliwania kwa mara tano kiti cha urais, baada ya kukaribia wadhifa huo wa juu mwaka wa 2008 alipoteuliwa kuwa waziri mkuu katika serikali ya mseto ya Hayati Rais Mwai Kibaki. 

Pamoja na masaibu yake ya kisiasa, Raila amesalia kuwa kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa hivi kwamba marais waliofuata wa Kenya walitatizika kuongoza kwa urahisi bila uungwaji mkono wake 

Pamoja na kutofanikiwa kushinda urais, alisifiwa kwa kusaidia kusambaratisha utawala wa chama kimoja cha Kenya chini ya Rais Daniel arap Moi mwaka 1992 na kupigania katiba mpya ya mwaka 2010, ambayo imeleta mageuzi makubwa ya kisiasa.

Yafuatayo ni mambo matano makuu kuhusu Raila.

1. Handishake’ na marais wote wa Kenya, isipokuwa Jomo Kenyatta.

Alifanya makubaliano – handshake – kwa  mara ya kwanza mwaka 1997, katika hatua ya kushangaza baada ya miaka mingi ya kuwekwa kizuizini na serikali ya Moi. 

Raila alikivunja chama chake cha National Development Party (NDP), ili kuungana na chama tawala cha KANU, ambapo alikabidhiwa wadhifa wa katibu mkuu wa chama hicho na wizara ya nishati.

Mkataba huo wa maelewano (MOU), ulikuwa mbinu ya Rais Moi kuendelea kuhudumu, lakini uliporomoka mwaka 2002 wakati Moi alipomtaja Uhuru Kenyatta, kama mrithi, hali iliomfanya Raila na viongozi wengine wengi kujiondoa serikalini na kusababisha kuzaliwa kwa chama cha Liberal Democratic Party (LDP). 

Mwaka 2008, alipeana mkono (handishake) na Rais Kibaki na akapewa wadhifa wa waziri mkuu kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi ambao ‘alidaiwa’ kushinda.

Mwaka 2018, alifanya handishake nyengine na Rais Uhuru Kenyatta baada ya matokeo ya uchaguzi uliopingwa na mahakama ambapo alisusia marejeleo yake yaliomfanya Uhuru kutangazwa mshindi. 

Katika uchaguzi wa 2022, baada ya kushindwa na William Ruto, Raila Odinga akaswa sehemu ya serikali pana.

Ruto alilazimika kubadili msimamo wake wa kutofanya majadiliano na Raila, baada ya kubainika kwamba uungwaji mkono wake hasa katika maeneo ya mkoa wa kati uliompigia kura kwa wingi kwenye uchaguzi uliopita (2022), ulikuwa umepungua kufuatia kuondolewa madarakani kwa kinara wa eneo hilo na aliyekuwa naibu Rais, Rigathi Gachagua.

Aidha, maandamano ya Gen Z yaliyosababisha Bunge kuvamiwa na vijana hao, yalimshinikiza Rais Ruto kumtafuta Raila kwa ushirikiano hatua iliosababisha kuundwa kwa serikali shirikishi au Broadbased Government-BG.

Handishake yake na Ruto ilimfanya Raila kuungwa mkono na serikali katika uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU), ambapo aligombea uenyekiti wa umoja huo. Akapatiwa nafasi za mawaziri katika serikali ya Kenya kwanza. 

2. Mapinduzi ya 1982 Kenya.

Saa 3 asubuhi ya Jumapili, tarehe 1 Agosti 1982, kikundi cha wanajeshi kutoka Jeshi la wanahewa la Kenya, wakiongozwa na Senior Private Hezekiah Ochuka, walijaribu kupindua serikali ya rais wa wakati huo, Daniel Arap Moi.

Baada ya jaribio hilo la kupindua serikali kufeli, Rais Moi alipanga upya usalama wa serikali yake na kuwaweka baadhi ya wandani wake. Akahakikisha Bunge linapitisha sheria inayompa mamlaka ya dharura huku akiweka utawala wa mkoa chini ya ofisi ya rais.

Wakati huo Raila Odinga alikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini baada ya kushutumiwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa mapinduzi hayo.

Alikaa gerezani kwa zaidi ya miaka sita. Aliachiwa Februari 1988 lakini akawekwa kizuizini tena Agosti mwaka huo huo na kuachiliwa tena Juni 1989.

Raila amewahi kuishi uhamishoni nje ya nchi.

3. Uchaguzi wa 2007 uliokumbwa na ghasia

Tarehe 27 Desemba 2007, uchaguzi mkuu ulifanyika nchini Kenya. Wapiga kura walimchagua Rais na wajumbe wa Bunge la Kitaifa. Uchaguzi huo pia uliambatana na uchaguzi wa mitaa Kenya.

Mwai Kibaki, aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Party of National Unity (PNU), alimshinda Raila Odinga, kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) na Kalonzo Musyoka wa Orange Democratic Movement–Kenya.

Uchaguzi huo ulikuwa na uhasama mkubwa wa kikabila, ambapo Kibaki aliungwa mkono na watu wa kabila lake la Wakikuyu naye Raila Odinga ambaye ni mtu kutoka kabila la Wajaluo akifanikiwa kuunda Muungano na viongozi kutoka makabila ya Magharibi, Bonde la Ufa, Pwani na kaskazini mwa Kenya.

Hata hivyo, Kibaki ndiye aliyetangazwa mshindi akiwa na asilimia 46 ya kura hizo na kuapishwa kuwa rais.

Raila Odinga alipinga matokeo hayo akidai kuwa yeye ndiye aliyeshinda uchaguzi huo. Hatua hiyo ilisababisha ghasia zilizosababisha mauaji ya raia huku zaidi ya watu lakini sita wakiachwa bila makao.

Hali hiyo lilihitimishwa na Sheria ya Makubaliano ya Kitaifa na Maridhiano, ambayo ilimfanya Raila kuteuliwa kuwa waziri mkuu 

Katika uchaguzi wa Bunge la Kitaifa, ODM ilishinda viti 99 kati ya 208, huku PNU ikimaliza ya pili kwa viti 43.

Bali kuna taarifa nyingine zinazodai kuna makubaliano katika jumuiya ya kimataifa kwamba uchaguzi huo wa urais ulichakachuliwa angalau kwa kiasi.

Mnamo Julai 2008, kura ya maoni iliyoidhinishwa na Marekani ilitolewa na kupendekeza kuwa Odinga alitabiriwa kushinda urais kwa tofauti ya asilimia 6, 46% hadi 40%, nje ya asilimia 1.3 ya makosa ya kura hiyo. 

4. Alijiapisha kama rais wa raia Kenya tarehe 30 Januari 2018.

Raila Odinga alikula kiapo kisicho rasmi cha “kuapishwa” kama rais wa raia licha ya vitisho kutoka kwa serikali kwamba angeshtakiwa na kosa la Uhaini wakati wa serikali ya Uhuru Kenyatta.

Odinga alikula kiapo chake akishangiliwa na maelfu ya wafuasi waliokuwa wamekusanyika katika bustani ya Uhuru Park, jijini Nairobi.

Wakati huo usalama katika mji mkuu wa Kenya ulikuwa umeimarishwa kabla ya sherehe hiyo huku mamlaka ikifunga vituo huru vya televisheni.

5. Raila alifahamu kuhusu kifo cha mama yake baada ya miezi miwili.

Waziri mkuu wa zamani wa Kenya, alifahamu kuhusu kifo cha mama yake, baada ya miezi miwili kupita.

Ni ukweli unaojulikana sana kutokana na wasifu wa Raila Odinga kwamba alifungwa gerezani mwaka 1982.

Alishutumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi mwaka huo huo. Mama yake Raila, Mary Juma Odinga, aliaga dunia miaka miwili baadaye mwaka 1984.

Raila Odinga aliyefungwa hakujulishwa kuhusu ukweli huu na akapata habari hiyo ya kusikitisha miezi miwili baadaye.

Aliachiliwa kutoka gerezani, tarehe 6 Februari 1988.

About The Author

error: Content is protected !!