
KAMATI ya Kitaifa inayoandaa Mazishi ya Kitaifa ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga imetangaza kwamba mazishi yake yatafanyika Jumapili nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya, magharibi mwa Kenya. Anaripoti Zakia Nanga Dar es Salaam … (endelea).
Naibu Rais Kithure Kindiki, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo pamoja na kaka yake mkubwa wa Odinga, Dk. Oburu Oginga, ametoa tangazo hilo katika hotuba ya kitaifa muda mfupi uliopita.
Kulingana na familia hiyo, Odinga aliomba kuzikwa ndani ya muda mfupi iwezekanavyo, ndani ya saa 72.
“Tumeamua kuharakisha mchakato wa maandalizi ya mazishi ya Odinga kwa kusawazisha matakwa ya Odinga, matakwa ya familia, jamii, na masharti mengine ambayo lazima izingatiwe,” kamati hiyo ilisema.
Mwili wa Raila Amolo Odinga umeshawasili Kenya hii leo tarehe 16 Oktoba 2025 kutoka nchini India.
Kutoka uwanjani JKIA, mwili umepelekwa moja kwa moja Lee Funeral Home Kutokana Wingi Wa Watu Waliojitokeza Kumuaga Mwanasiasa Huyo Mkongwe Wa Kenya Mwili Wake utapelekwa Katika Uwanja Wa Kasarani,ambapo Wakenya watapata furda ya kutoa heshima zao za mwisho kuanzia saa sita mchana.
Baadaye, mwili utarudishwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee Funeral Home kwa maandalizi ya mwisho.
Ijumaa, ibada ya kitaifa ya mazishi itafanyika katika Uwanja wa Nyayo.
Viongozi kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo, ambayo itasimamiwa kama ibada rasmi ya kitaifa.
Jioni ya siku hiyo, mwili utafikishwa nyumbani kwake Karen ambapo utalazwa kwa mara ya mwisho.
Jumamosi, mwili utasafirishwa hadi Uwanja wa Moi, Kisumu, ambapo wananchi wataruhusiwa kuuaga kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri.
Kutoka hapo, msafara wa mazishi utaelekea kwa barabara hadi Siaya. Maziko yatafanyika Jumapili nyumbani kwake Bondo.
ZINAZOFANANA
Raila Odinga afariki dunia
Uhamiaji yawang’ang’ania wageni wa Lissu
Bunge la Peru lamuondoa rais wake madarakani