
Félicien Kabuga
MAHAKAMA ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), iliyosalia kusikiliza kesi zilizoachwa na Mahakama hiyo mjini Arusha, huenda ikamrejesha nchini mwake, Felicien Kabuga. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Mwendesha mashitaka wa Kitengo cha mahakama hiyo, ameomba kufanyike utafiti wa kuachiwa kwa muda kwa Kabuga na kuhamishiwa Rwanda.
Amesema, Kabuga amezaliwa nchini Rwanda na “ndio nchi pekee ilionyesha nia ya kumpokea,” kwa mujibu wa waraka kutoka katika kitengo hicho.
Kwa sasa Kabuga anazuiliwa katika gerezani mjini Hague, nchini Uholanzi, baada ya taasisi moja inayofanya kazi zake nchini humo, kuamua Septemba mwaka jana, kusitisha kwa muda usiojulikana kesi dhidi yake.
Kabuga mwenye umri wa miaka 90 ameelezwa kuwa hali ya afya yake siyo mzuri, na kwamba huenda akaachiliwa kwa dhamana.
Anashitakiwa kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kifedha kwa mauaji ya Kimbari ya 1994 nchini mwake, mashtaka aliyoyaita “uongo mtupu.”
Juzi Jumanne, jopo la majaji watatu – Iain Bonomy, Mustapha El Baaj na Margaret M. deGuzman na msajiliwa wa mahakama hiyo, Abubacarr Tambadou, walikutana mjini Arusha na kujadili kuhusu kuachiliwa kwa muda kwa Kabuga na kurejeshwa nchini Rwanda.
Hati hiyo ya mahakama inasema, kutokana na matukio ya miaka miwili iliyopita, “Kabuga akiachiliwa atakwenda Rwanda pekee.”
Redio ya Ufaransa (RFI), inaripoti kwamba wakili wa Kabuga alijaribu kuuliza moja ya nchi za Ulaya kumkubali.
Hata Ufaransa, nchi ambayo alikamatwa Mei 2020, baada ya miaka 26 ya kuwa mafichoni, taarifa zinasema, “bado haijakubali kumpokea.”
Mfanyabiashara huyo tajiri aliwakwepa waendesha mashtaka waliokuwa wakichunguza mauaji ya kimbari nchini Rwanda kwa zaidi ya miongo miwili na nusu kwa kutumia majina 28 tofauti ya watu maarufu katika mabara mawili ili kutofikiwa na mkono wa sheria.
Mzee huyo aliishi mafichoni kwa muda mrefu, jambo lililosababisha jopo la kimataifa lililobuniwa kuchunguza mauaji hayo, liliacha kufanya kazi yake.
Hatimaye alisakwa katika maficho yake katika kijiji kimoja cha mji mkuu wa Ufaransa na kupatikana kufuatia uchunguzi ulioanzishwa na Serge Brammerts, mwendesha mashtaka wa Umoja wa Mataifa (UN), akiongoza jopo linalosimamia uhalifu wa kivita nchini Rwanda na Yugoslavia.
”Tulijua mwaka mmoja uliopita, kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa yeye kuwa nchini Uingereza, Ufaransa ama Ubelgiji na tuliamua miezi miwili iliopita kwamba alikuwa nchini Ufaransa,” alieleza mwendesha mkuu wa jopo hilo la uchunguzi.
Alisema, serikali ya Ufaransa iliwaonyesha nyumba aliyokuwa anaishi mtuhumiwa huyo kama maficho, hatua iliyosababisha operesheni hiyo.
Mojawapo ya sababu kuu kwanini alifanikiwa kutoroka kwa muda mrefu, ni kujitenga na watoto wake.
Anajulikana kuwa na watoto watano – watoto wake wawili walikuwa wameolewa na watoto wa aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana, ambaye kifo chake baada ya ndege yake kuangushwa tarehe 6 Aprili 1994 kilisababisha mauaji hayo ya kimbari.
Wachunguzi wa Kimataifa waliwachunguza watoto wake ili kubaini anakoishi baba yao, ambapo alikuwa anaishi kwa kutumia pasipoti kutoka kwenye taifa la Afrika lisilojulikana.
Kulingana na kanali Eric Emaraux, anayeongoza kitengo maalum cha polisi katika kukabiliana na uhalifu, mlipuko wa virusi vya corona pia ulisadia kwasababu amri ya kutotoka nje ilisitisha operesheni nyingi katika maeneo mengi ya Ulaya, na hivyo kutoa fursa ya kumsaka mtu anayedaiwa alikuwa mfadhili mkuu wa mauaji ya kimbari.
Katika siku 100 pekee mwaka 1994, takriban watu 800,000 waliuawa nchini Rwanda na watu wa kabila la Wahutu ambao bwana Kabuga, mfanyabiashara ambaye alikuwa amejinufaisha kupitia sekta ya majani chai aliwaunga mkono.
Walikuwa wakiwalenga watu wasio wengi wa jamii ya Watutsi, pamoja na wapinzani wa kisiasa bila kuchagua kabila lao.
Marekani ilikuwa imetoa zawadi ya doza 5 milioni, kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazosababisha kukamatwa kwa Kabuga.
Lakini ilikuwa inashangaza kwamba kwa miaka mingi mtu aliyekuwa anatafutwa sana Afrika, baada ya kushtakiwa kwa makosa saba ya mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu 1997, alifanikiwa kuishi mafichoni na kukwepa mkono wa sheria katika mataifa na mabara.
ZINAZOFANANA
Mke wa Rais Ivory Coast ajitosa kwenye mbio za urais
Mike Tyson kurudi ulingoni na Mayweather 2026
Rais mstaafu Peru ahukumiwa miaka 13 jela