
ALIYEKUWA rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, anayeshitakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhusiano wake na kundi la waasi la M23, “anastahili kunyongwa.” Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Waendesha mashitaka nchini humo, wameomba rais wa zamani ahukumiwe adhabu ya kifo kwa makosa ya uhaini katika kesi inayomkabili mahakamani.
Jenerali Lucien René Likulia, aliyemwakilisha mwendesha mashtaka nchini humo ameitaka Mahakama, jana Ijumaa, tarehe 22 Agosti, kumtia hatiani Kabila na kumpatia adhabu ya kifo.
Mbali na adhabu ya kifo, Likulia ametaka mahakama imhukumu Kabila kifungo cha miaka 20 gerezani kwa madai ya kufumbia macho uhalifu wa vita na miaka 15 mengine kwa kula njama na wahalifu.
Hata hivyo, kesi dhidi ya Kabila inaendelea bila ya yeye kuwepo mahakamani. Anatuhumiwa kwa makosa ya uhaini, mauaji na ubakaji, pamoja na makosa mengine ya uhalifu wa kivita.
Wafuasi wake wanasema, kesi hiyo inaendeshwa kwa kutumia nguvu za kisiasa, ndio maana rais wa zamani aliondolewa kinga ya urais, Mei mwaka huu.
Mpaka sasa, Kabila hajulikani alipo. Lakini mwaka 2024, Rais Felix Tshisekedi alimshutumu mtangulizi wake huyo kwa kuwaunga mkono waasi na “kushirikiana nao katika kutayarisha uasi, madai ambayo mwanasiasa huyo ameyakana.
Chama chake cha PPRD, kinachoongozwa na Ferdinand Kambere, waziri wa zamani chini ya utawala wa Kabila kimesema, kufutiwa kinga rais huyo wa zamani ilikuwa ndio mwanzo wa kampeni chafu dhidi yake.
Henry-Pacifique Mayala, mtafiti na mratibu wa shirika la Ufuatiliaji wa Usalama la Kivu ameliambia shirika la Habari la AP kwamba madai ya mwendesha mashtaka yanaonekana kuwa “zaidi ya kutafuta alama za ushindi kuliko kutafuta ukweli.”
Kabila aliyeiongoza Kongo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, akiwa na miaka 19, amefunguliwa mashtaka hayo tangu Julai mwaka jana.
Serikali ya Kongo pia imedai kuwa kiongozi huyo wa zamani analiunga mkono kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Alichukua madaraka baada ya baba yake Laurent Kabila kuuwawa na alirefusha uongozi wake kwa kuchelewesha uchaguzi kwa muda wa miaka miwili baada ya muda wake kumalizika mwaka 2017.
Kundi la M23 ndio wanadhibiti miji miwili muhimu ya eneo la mashariki ya Goma na Bukavu nchini Kongo.
Bado hakujatolewa tarehe rasmi ambapo mahakama itatoa uamuzi wa kesi hiyo.
Kabila alikuwa anaishi uhamishoni tangu mwaka 2023 hadi mwezi Aprili 2025, alipowasili katika mji wa Goma unaodhibitiwa na waasi baada ya mji huo kutekwa na waasi hao.
ZINAZOFANANA
Waaandamanaji waingia mtaani kumpinga Netanyahu
Watu 18 wafa kwa njaa Ukanda wa Gaza
Vita vya Gaza: Hamas waapa kufia kwenye ardhi yao